Uimarishwaji wa Umaizi Mseto Kupitia Mikakati Shirikishi ya Ufundishaji wa Kiswahili Nchini Kenya
Ombito Elizabeth Khalili
lwangakhalili@gmail.com
Rongo University, Kenya
Ikisiri
Upataji wa elimu na maarifa ni shughuli isiyo na kikomo katika maisha ya mwanadamu. Ili kuimarisha shughuli hii, lengo la nne la Maendeleo Endelevu linamhitaji kila mwanafunzi kutoachwa nyuma kwenye ujifunzaji na upataji wa maarifa. Lugha ni chombo muhimu katika ufundishaji na ujifunzaji wa somo lolote lile. Hivyo basi, ipo haja ya kumwelekeza mwanafunzi kufikia viwango toshelevu vya umilisi wa lugha, kama chombo cha kujipatia elimu na maarifa ya kudumu maishani. Nadharia ya umaizi mseto, iliyoasisiwa na Howard Gardner inatambua kuwepo kwa aina tofautitofauti za vipawa katika kikundi cha wanafunzi. Vipawa hivi vinastahili kupaliliwa na kukuzwa kwa kutumia mikakati tofautitofauti inayomshirikisha kila mwanafunzi. Naye Lev Vygotsky anapendekeza kutumika kwa mfululizo wa mikakati ya kumwimarisha kila mwanafunzi ili afikie kilele cha matamanio yake kielimu. Ili kuchochea ukuaji wa vipawa na kumshirikisha kila mwanafunzi kwenye somo, mwalimu analazimika kuteuwa na kutumia mikakati kadha anapofundisha. Makala haya yanatathmini mbinu, mikakati na nyenzo shirikishi zinazofaa kutumika katika ufundishwaji wa Kiswahili kwa lengo la kukuza kipawa cha kila mwanafunzi darasani. Mikakati yenyewe inajadiliwa kwa kuangazia utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu nchini Kenya, unaopendekezwa kutumika kuanzia mwaka 2019. Mjadala kwenye makala haya unalenga kujenga uhusiano kati ya nadharia na utekelezwaji wake kwenye shughuli za ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili kama wenzo wa kutimiza malengo ya kitaifa na ya kimataifa kuhusu elimu.
Maneno muhimu: ufundishaji, mikakati shirikishi, umaizi mseto.
Utangulizi
Kaulimbiu ya Malengo Endelevu ni ‘Kutomwacha mtu yeyote nyuma’. Hii ina maana kuwa mikakati yoyote ya kuleta maendeleleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi sharti iwashirikishe washika dau wote ili kuwepo ufanisi unaoaminika na wa kudhihirika. Mataifa mengi ulimwenguni yametambua umuhimu wa kuwashughulikia raia wake kwa pamoja, licha ya tofauti zao za kimaumbile, kimazingira, kidini na za kiuchumi. Kushirikishwa huku kunalenga kupunguza umaskini, makali ya njaa, kuimarisha viwango vya afya, elimu, ajira na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo (United Nations, 2016). Elimu inatambuliwa kuwa chombo muhimu cha kuzingatisha maarifa, kubadili mitazamo hasi, kukuza tafakari na kuleta uvumbuzi wa kuboresha maisha ya binadamu. Kati ya Malengo Endelevu, lengo la nne ni kuwezesha upataji wa stadi za kimsingi na za kiwango cha juu cha maarifa, yakiwemo ya kiufundi na ya kitaaluma.Upataji wa maarifa haya unapaswa kendelezwa katika maisha ya mwanadamu bila kikomo.
Mbali na maarifa, elimu inatarajiwa kumzingatisha mwanadamu stadi na amali maalum ili kumwezesha kuishi vema na kuchangia utatuzi wa mambo ndipo maendeleleo yapatikane. Mchakato wa utatuzi wa mambo unashirikisha utumiaji wa umaizi na tafakari ili kuhamisha maarifa na stadi alizo nazo mtu, kwa kufanya maamuzi au vitendo vinavyoweza kusuluhisha matatizo katika jamii. Lugha, kama chombo cha mawasiliano, humwezesha mtu kupata maarifa mapya, stadi na mbinu za kumwezesha kuishi na kutagusana na mazingira yake. Hivyo basi pana umuhimu wa kujifunza lugha kwa njia zinazoimarisha mawasiliano, utangamano, umakinifu, udadisi na utendaji katika maisha ya mwanafunzi.
Kiswahili ni Lingua Franca barani Afrika. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kiswahili ndiyo lugha inayotambulishwa zaidi na utamaduni, amali na siasa za kijamii. Kwenye mitaala ya elimu, Kiswahili ni somo la kumzingatisha mwanafunzi stadi na kaida za mawasiliano katika miktadha mbalimbali ya maisha ya jamii kama vile biashara, michezo, kwenye viwanda vya Jua Kali, maabadini, kwenye ulingo wa kisiasa na katika hafla za kitamaduni. Jumuiya ya Afrika Mashariki imependekeza kuwa mitaala ya elimu kwa mataifa wanachama inapaswa:
- Kutelekezwa kwa mwelekeo unaomlenga zaidi mwanafunzi kwa kuseta hali, matamanio, ilhamu na uwezo wake, mbali na kuhimiza haki za kibanadamu.
- Kuweka wazi aina za uwezo unaolengwa kuimarishwa kwa mwanafunzi na kutaja namna ya kutathmini kutimizwa kwa uwezo huo.
- Kuimarisha ufundishaji kwa mwelekeo mseto ili kujenga uhusiano kati ya masomo tofautitofauti, kuhusisha maarifa na mazingira, kukuza mchango wa mwanafunzi kwa ujifunzaji na kuwezesha upokezi wa maarifa kwa umoja wake.
- Kuimarisha vipawa vya kila mwanafunzi, kuvitumia vipawa hivyo kwa upataji wa maarifa na kuvikuza ili kukidhi matamanio na mahitaji ya kila mwanafunzi.
(East African Community, 2014)
Kwa ufupi, mitaala ya elimu katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inalenga kumshirikisha mwanafunzi kwa kuchakata, kupata na kutumia maarifa ili kutatua migogoro, majanga na umaskini kwenye jamii ndipo maendeleo yanawiri. Ufundishaji wa Kiswahili kama somo la lazima unafaa kumwezesha mwanafunzi kutimiza ndoto alizo nazo kuhusu vipawa vyake na kumtimizia matarajio yake maishani ili aishi kwa amani.
Kwa wanafunzi wengi nchini Kenya, Kiswahili ni lugha yao ya pili kutokana na urasmi wa kufundiswa shuleni kama somo la lazima. Aghalabu, mwanafunzi huja shuleni akiwa tayari na maarifa kuhusu lugha ya kwanza ambayo ndiyo lugha-mama. Kwa maoni ya Vygotsky, ujifunzaji wa mtoto huanzia nyumbani. Yale ajifunzayo shuleni humkuta akiwa tayari na maarifa ya awali kama vile kuhesabu, kugawa, kuongeza, kuitika, kusalimu na kujieleza (Vygostky, 1978). Ni jukumu la mwalimu wa Kiswahili kubaini kiwango cha ukuaji wa mwanafunzi ili aratibu mafunzo ya mtaala yanayoweza kupokelewa na kufasiriwa na mwanafunzi wa kiwango hicho. Hata hivyo, kiwango cha ukuaji wa akili ya mtoto si kizingiti kwa uwezo wa kujifunza maarifa yaliyozidi kiwango hicho. Pana uwezekano wa mtoto wa kiwango fulani cha ukuaji kujifunza na kutekeleza maarifa zaidi ya kiwango chake kwa kusaidiwa, kuchangiwa na kuimarishwa na mwalimu au wanafunzi wenza. Vygotsky (keshatajwa) anakiita kiwango hiki cha juu cha maarifa kuwa ‘Eneo la Kilele cha Ukuaji’.
Makala haya yanatathmini mikakati ya kufunza Kiswahili kwa mtaala mpya wa shule za upili nchini Kenya kwa kuzingatia nadharia ya umaizi mseto ili kumshirikisha mwanafunzi na kupalilia vipawa vyake (Kenya Institute of Curriculum Development, 2017). Ufundishaji unaohimizwa ni ule unaomwezesha mwanafunzi kufikia matamanio yake na hasa eneo la kilele cha ukuaji. Sehemu ya kwanza ya makala haya inafafanua nadharia ya umaizi mseto kwa mujibu wa Howard Gardner (1993). Uhusiano wa nadharia hii na ufundishaji wa Kiswahili kwa lengo la kutimiza Malengo Endelevu unabainishwa pia. Katika sehemu ya pili, vipengele vya mtaala mpya unaosistiza uimarishwaji wa vipawa, vinajadiliwa. Mielekeo inayochangia utekelezwaji wa mtaala mpya wa Kiswahili inatathminiwa. Hii ni pamoja na ufundishaji kwa mwelekeo wa kimawasiliano, mwelekeo wa kimajukumu na mwelekeo mseto. Mielekeo hii ina mchango mkubwa kwa kuimarisha utendaji, ubunifu, kujiamini na utumiaji wa maarifa aliyo nayo mwanafunzi kwa utatuzi wa mambo.
Kiini cha makala haya ni kubaini mikakati shirikishi inayochangia ukuaji wa vipawa vya wanafunzi. Sehemu ya tatu inapambanua mikakati ya kumfikisha mwanafunzi kwenye eneo la kilele cha ukuaji. Mikakati hii ni pamoja na ufundishaji wa vitendo, ufundishaji wa kuongozwa, kazi mradi, utatuzi wa mambo na vikundi kama njia ya kuwezesha kutimizwa kwa Malengo Endelevu.
Nadharia ya Umaizi Mseto kwa Ufundishaji wa Kiswahili
Dhana ya umaizi inafafanuliwa kwa njia mbalimbali kutegemea wasomi. Kamusi Kuu ya Kiswahili inafafanua umaizi kuwa ni “Uwezo wa kubaini au kufahamu jambo fulani”(Baraza la Kiswahili la Taifa, 2015). Katika ujifunzaji, umaizi ni uwezo alio nao mwanafunzi wa kutambua, kutumia na kufasiri maana ya maneno katika lugha. Umaizi pia unaweza kuchukuliwa kuwa uwezo alio nao mtu, wa kufahamu jambo au maarifa kuhusu taaluma fulani (Koenig, 2009). Lakini, umaizi ni zaidi ya utambuzi au ufahamu wa dhana na maarifa. Gardner (keshatajwa) anaongeza kuwa umaizi ni uwezo wa kuunda na kusuluhisha matatizo, kuunda vitu au kutoa huduma zinazothaminiwa katika utamaduni fulani au jamii (Zhou, 2014). Kutokana na vijelezi hivi, umaizi mseto ni dhana inayorejelea kuwepo kwa zaidi ya aina moja ya uwezo. Uwezo huu ni wa kuzaliwa nao na humwezesha mwanafunzi kupata maarifa mapya, kuyafasiri akilini, kuyahusisha na maarifa ya awali, kuyahifadhi na kuyatumia katika utatuzi wa mambo. Baadhi ya matatizo yanayohitaji kusuluhishwa katika ujifunzaji wa lugha ni kudumisha mawasiliano kama vile kujuliana hali, kutoa maoni kuhusu masuala ibuka, kuandaa ilani kwa madereva kuhusu kuporomoka kwa barabara kutokana na mafuriko, kuendeleza mjadala kuhusu uhasama wa kisiasa, kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kuzuia mkurupuko wa maradhi; miongoni mwa masuala mengine mengi. Utatuzi wa mambo haya unamhitaji mwanafunzi kuwa na ufahamu wa kina kuhusu lugha kama vile sarufi, msamiati, kaida za matumizi, sajili maalum na dhima zinazotekelezwa na lugha. Dhima hizi ni kama vile: kuwasiliana, kukuza uhusiano mwema, kuonya, kutambulisha jamii, kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii; miongoni mwa nyingine.
Nadharia ya umaizi mseto inajumuisha aina nane za umaizi. Kabla ya kutaja aina nane za umaizi ni muhimu kuweka wazi machu kulio ya Gardner katika nadharia hii. Kulingna na Zhou (2014) kuna mihimili ifuatayo ya umaizi mseto:
- Kila binadamu anamiliki aina zote za umaizi, japo kwa viwango tafauti.
- Kila binadamu ana aina moja kuu ya umaizi inayomtambulisha na kumfanya apendelee kuitumia zaidi katika upataji wa maarifa kuliko aina nyingine.
- Ujifunzaji wa maarifa yoyote unaweza kuboreshwa ikiwa mwalimu atakadiria umaizi unaomtambulisha kila mwanafunzi katika darasa lake; na kupanga mikakati inayomlenga ya kufundishia.
- Kila aina ya umaizi imetengewa sehemu maalum katika ubongo wa binadamu.
- Aina zote nane za umaizi zinaweza kuchangiana na kuimarishana kwa pamoja au kila aina ya umaizi itumike pekee yake wakati wa kujifunza.
- Pana uwezekano wa kuwaainisha wanadamu kwa kutumia mitindo wanayopendelea katika kujifunza maarifa na stadi.
Machukulio ya Gardner ni kuwa kila binadamu huzaliwa akiwa na uwezo wa kujifunza maarifa ikiwemo lugha. Mitindo ya kujifunza ndiyo inayotofautisha watu na kuamua kasi ya ujifunzaji. Hata hivyo, ujifunzaji unaathiriwa na mambo mengi, mbali na umaizi na mitindo ya kujifunzia. Katika makala haya, ninasistiza ujifunzaji wa lugha unaolenga kuboresha stadi za mawasiliano, ambazo aghalabu mtoto hujifunza bila hiari, hasa anapozibwia kutoka kwa mazingira yake. Kawaida ya binadamu ya kutaka kuwasiliana na mwenzake humchochea kubwia lugha ya kwanza kwa kusikiliza, kuiga na kutenda; bila mafunzo rasmi. Mtoto anapofika shuleni na kufundishwa Kiswahili kama lugha ya pili, anatarajiwa kutumia aina zifuatazo za umaizi kulingana na Gardner (1993):
- Umaizi wa kimatamshi au wa kiisimu.
Huu ni uwezo wa kuelewa na kutumia lugha kupitia kwa stadi za kusikiliza, kuongea, kusoma na kuandika. Umaizi huu humpa utambuzi na utumiaji wa lugha-matamshi na lugha-andishi. Ingawa umaizi wa kimatamshi huchukuliwa kuwa uwezo wa kimsingi kwa mtoto yeyote asiye na ulemavu wa kimaumbile, baadhi ya wanafunzi hupendelea kujifunza kwa kumsikiliza mwalimu, kujieleza kwa maneno, kuandika na kuwasilisha tungo mbalimbali. Wanafunzi wenye umaizi wa kimatamshi wanaweza kupangiwa shughuli za ujifunzaji kama vile kuandaa na kutumia shajara, kucheza michezo ya kujenga maneno, vitanza ndimi, kushiriki kwa mijadala na kutunga na kuhakiki kazi za kifasihi.
- Umaizi wa kihisabati
Mwanafunzi mwenye umaizi wa kihisabati huchukuliwa kuwa mwenye uwezo wa kukusanya, kupanga, kuchanganua na kufasiri data ili kupata maana fiche na kuitumia kufikia maamuzi au kauli fulani. Umaizi huu humwezesha mwanafunzi kuona uhusiano baina ya matukio au hali tofauti kwenye mazingira na kuunda ruwaza ya kuelezea uhusiano huo. Shughuli za ujifunzaji zinazomvutia mwanafunzi anayeegemea umaizi wa kihisabati ni kama: majedwali yenye data za kumfikirisha; ruwaza za kidhahania kuhusu dhana za kisayansi na kutumia data za kinumerali kusuluhisha mambo. Mwalimu anashauriwa kutumia data za tarakilishi, chemsha bongo na shughuli zinazohitaji umakinifu wa fikra ili kumshirikisha mwanafunzi anayetambulishwa kwa umaizi wa kihisabati.
- Aina ya nne ni umaizi wa kimisuli. Kulingana na Koenig (2009) mwanafunzi aliye na umaizi wa kimisuli hupendelea kupokea maarifa kwa kutumia viungo vya mwili wake kugusa, kuigiza, kujiundia vifaa au kufanya ujarabati wa dhana kwenye maabara. Aliye na umaizi wa kimisuli pia hupendelea kushiriki kwa shughuli za michezo au kuzungumza kwa kushirikisha miondoko ya kimwili (Gardner, 1993). Katika ufundishaji wa Kiswahili, ni muhimu mwalimu ampe mwanafunzi fursa ya kujieleza akitumia viziada lugha kwenye maigizo au uigizaji bubu.
- Umaizi wa kimuziki huelekeza fikra za mwanafunzi kubaini mapigo ya sauti yanayojirudia na kuunda mkarara. Wanafunzi waliokoleza umaizi wa kimuziki hupendelea kuimba, kupiga mluzi, kucheza ala za muziki na kujitungia nyimbo na mashairi. Aghalabu, umaizi huu hutambulika mapema utotoni kwa sababu watoto wengi hupendelea kuimba, isipokuwa wale wenye ulemavu wa masikizi. Mwalimu wa Kiswahili anashauriwa kutumia nyimbo, maghani na mashairi andishi kutanguliza, kuendeleza au kuhitimisha somo. Ni vizuri ikiwa wanafunzi walio na vipawa hivi watashirikishwa kutunga, kukariri, kufoka au kuimba nyimbo zao darasani wakati wa somo la Kiswahili.
- Baadhi ya wanafunzi hudhihirisha mno umaizi wa mazingira halisi. Ujifunzaji wao huboreshwa zaidi wanapotoka nje ya darasa na kuzuru eneo lenye mazingira halisi kama vile mlima, mto, mbuga ya wanyama, chimbo la mawe au msitu. Wanapotambulisha wanyama na mimea katika mandhari yao, wao huona mazingira kuwa eneo la kuzalisha maarifa kwa umoja wake. Ili kushirikisha umaizi wa kimazingira, mwalimu anaweza kutumia mbinu ya ziara nyanjani, kazi mradi au kutumia nyenzo halisi kama vile video za maeneo maalum, mimea, matunda au wanyama kufunza mada kuhusu sarufi ya Kiswahili.
- Umaizi wa kimtagusano ni uwezo wa mwanafunzi kufasiri na kupokea hisia, himizo, hali na matendo ya watu wengine. Kwa mujibu wa Ellis (2003) mwalimu anahitajika kuwapa wanafunzi majukumu yanayohimiza kusaidiana na kuchangiana maarifa. Katika ufundishaji wa Kiswahili, majukumu ya kimakundi yanaweza kutumika kwenye utafiti wa maktabani, kazi mradi au mahojiano ya kupata maoni ya watu tofauti kuhusu sera mpya za elimu. Koenig (2009) anaongeza kuwa wanafunzi walio na kiwango kikubwa cha umaizi wa kimtagusano hupendelea kuwasikiliza wengine wakitoa maoni, kushauriana na kupanga shughuli zinazowezesha ushirikiano katika mazingira ya ujifunzaji. Aghalabu wanafunzi hao huwa na vipawa vya uongozi.
- Wanafunzi wengine hupendelea kujifunza maarifa wenyewe. Wao hujielewa kihisia, wanafahamu ubora na udhaifu wao. Wanajua wanachokitamani kutelekeza masomoni na hupenda kutafakari, kuchanganua dhana na kujitathmini wenyewe. Huu ni umaizi nafsi, unaomwezeha mwanafunzi kujipangia utaratibu wake wa kujisomea, kufatiti, kufanya mijarabu na kujipima weledi wake wa dhana. Aghalabu, wanafunzi wenye umaizi wa nafsi hawapendi kushirikishwa kwa vikundi. Aina hii ya umaizi hujumuisha aina nyinginezo ili kumwezesha mwanafunzi kuwa na msukumo wa kibinafsi wa kuchakata maarifa.
- Umaizi wa kiutazamaji ni uwezo wa kujiundia maarifa kwa kujichorea picha au maumbo ya dhana akilini (Richards na Schmidt, 2010). Wanafunzi wenye umaizi wa kiutazamaji hujipatia maarifa kwa kutazama nyenzo kama vile picha, michoro, filamu, video, michongo ya kisanaa na mbinu ya maonyesho. Wanafunzi hawa hujieleza vema zaidi kupitia kwa sanaa kama vile uchoraji, ufinyanzi, uchongaji wa sanamu na uundaji wa maumbo. Wanapendelea kufikiri kwa kuunda picha akilini, kubuni na kuigiza, kusoma ramani na kufumbua mafumbo. Sehemu ya ubongo wao inayotumika zaidi ni ya upande wa kulia (Gardner, 1993). Mwalimu wa Kiswahili anashauriwa kutumia nyenzo za kisanii kama michoro, na kuwashirikisha kutumia sanaa zenye nakshi kwenye tarakilishi kuandaa nyenzo za kujifunzia.
Nafasi ya Nadharia ya Umaizi Mseto kwenye Mtaala Mpya wa Elimu
Tathmini iliyofanywa mwaka wa 2009 kuhusu mtaala wa mfumo wa elimu wa 8-4-4 ilibaini kuwa mfumo huo haukuruhusu kwa urahisi, mabadiliko ya kutambua na kukuza vipawa vya mwanafunzi mapema, ili kumwandaa kwa utekelezwaji wa ajira kulingana na ilhamu zake (Republic of Kenya, 2010). Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo, mfumo wa elimu ulisistiza zaidi mwanafunzi kupita mitihani ya kitaifa ili aweze kuendelea na masomo. Matokeo bora ya mitihani yalichukuliwa kuwa kipimo cha kipekee cha kukadiria ufanisi na upataji wa ajira. Ushindani wa alama za juu kwenye mitihani ulihusishwa na kudorora kwa maadili ya kiusomi na kuchangia uozo wa maadili ya kitaifa. Kamati ikateuliwa ili kuratibu upya sekta ya elimu kulingana na ruwaza ya Kenya Vision 2030 na katiba ya Kenya 2010. Serikali ilitoa tamko rasmi kuhusu mabadiliko ya elimu na mafunzo kwa kusema kuwa:
- Mfumo wa elimu uelekezwe na falsafa ya kitaifa.
- Mabadiliko yafanyiwe sekta ya elimu na mafunzo ili kukuza uwezo wa kila mwanafunzi.
- Mwanafunzi akuzwe kwa mwelekeo mseto ili kumuimarisha kiusomi, kihisia, na kimaumbile ndipo akuwe kikamilifu.
- Mtaala mpya uangazie ukuzaji wa vipawa na kushirikishwa kwa aina tofauti za umaizi.
- Kuanzishwe mfumo wa kitaifa wa kutathmini ujifunzaji.
- Mfumo wa elimu uhimize utambuzi na ukuzaji wa vipawa vya mwanafunzi mapema.
- Kuingizwa kwa maadili na mshikamano wa kitaifa kwenye mtaala.
- Kuanzishwa kwa mikondo mitatu ya ujifunzaji katika kiwango cha juu cha elimu ya shule za upili.
(Republic of Kenya, 2012)
Ruwaza hii iliwaelekeza washika dau kuteuwa nadharia bunilizi za ufundishaji na ujifunzaji, ikiwemo nadharia ya umaizi mseto. Masomo ya Lugha na Fasihi ya Kiswahili yanapaswa kufunzwa kwa mwelekeo mseto ili kumpa mwanafunzi nafasi ya kutagusana na mazingira yake na kujitambulisha nayo. Mikakati inayoruhusu utendaji wa mwanafunzi inapendekezwa itumike ili kuchangia utekelezwaji wa nadharia ya umaizi mseto. Katika awamu ya pili ya elimu ya sekondari, Kiswahili kitafunzwa kama masomo mawili- Lugha na Fasihi. Lugha ya Kiswahili itamhitaji mwanafunzi kujifunza aina na miktadha mbalimbali ya mawasiliano; aina tofauti za uandishi; aina za usomaji na uhakiki wa makala ya ufahamu. Pia mwanafunzi atajifunza sarufi pamoja na misingi ya tafsiri. Mafunzo haya yanalenga kumwandaa mwanafunzi kujiunga na taaluma kama vile: burudani, uanahabari, uandishi, ukalimani, ualimu na siasa (Kenya Institute of Curriculum Development, 2017).
Somo la Fasihi ya Kiswahili nalo litampa mwanafunzi fursa ya kujifunza fasihi simulizi; fasihi andishi; uhakiki wa tanzu mbalimbali za fasihi andishi; kutazama maigizo ya kazi za fasihi; kutazama mijadala ya uhakiki wa fasihi; kushiriki kwenye tamasha za uigizaji; kufanya utafiti na kazi mradi kuhusu fasihi simulizi; kushiriki kwa mijadala inayoshirikisha shule mbalimbali kuhusu uhakiki wa vitabu teule vya fasihi. Lengo la kufunza Kiswahili kwa mtaala mpya ni kuimarisha uwezo wa kuwasiliana; kuthamini maadili ya kijamii, na kukuza uwezo wa mwanafunzi wa kutumia lugha kwa manufaa ya kibinafsi na ya kijamii. Ili kutimiza lengo hili, nadharia ya umaizi mseto inafaa zaidi kutumiwa katika ufundishaji unaomlenga na kumshirikisha mwanafunzi.
Mbali na masomo ya lugha, umaizi mseto unaweza kutumiwa kujifunza maarifa na stadi maalum katika masomo ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano; Huduma kwa Jamii; Sheria na masuala ya kimaadili; Sanaa za maonyesho; Sayansi za michezo na ufundi. Masomo ya aina mbalimbali yameteuliwa na kuingizwa kwenye mtaala mpya ili kushirikisha kila aina ya uwezo na ilhamu ya mwanafunzi katika kutimiza Malengo Endelevu yanayohusu umaskini, njaa, mazingira na afya , ajira pamoja na elimu. Ili kuteuwa mikakati shirikishi ya kufunzia Kiswahili, mwalimu anastahili kuwa na ufahamu kuhusu mielekeo bunilizi ya kutekeleza mtaala mpya.
Mielekeo ya Kufundishia Mtaala Mpya wa Kiswahili
Hakuna mwelekeo mmoja unaoweza kutumika kwa kukuza umaizi mseto katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili. Katika kuteuwa mwelekeo wa kufundishia, mwalimu anapaswa kuzingatia shughuli zinazoweza kutekelezwa na mwanafunzi ili kuchangia umilisi na ustawishaji wa mawasiliano kwenye miktadha mbalimbali. Ni muhimu pia kuteuwa mwelekeo unaomzingatisha mwanafunzi mbinu za kutagusana na mazingira yake katika: kuwasiliana; ukusanyaji wa data za kifasihi; uchanganuzi na uhakiki wa masuala ibuka na yale ya fasihi; kuigiza na kutafsiri matini mbalimbali yakiwemo yale ya fasihi za lugha nyingine. Ili kutimiza malengo haya, ninapendekeza Kiswahili kifunzwe kwa kuzingatia mielekeo mitatu- mwelekeo wa kimawasiliano; mwelekeo wa kimajukumu na mwelekeo mseto.
- Mwelekeo wa Kimawasiliano
Unajumuisha mapendekezo ya nadharia kutoka kwa taaluma mbalimbali kama vile: Isimu, Saikolojia, Anthroplojia, Pragmatiki na Uchanganuzi wa usemi (Kumaravadivelu, 2006). Mtazamo huu ulichangiwa zaidi na wanaisimu kama vile: Noam Chomsky, Michael Halliday, Dell Hymes na Austin. Chomsky anachukulia lugha kuwa mfumo wa mageuzi, unaoruhusu ubunifu na upekee wa mtu kimatumizi. Halliday naye anaongeza kuwa ujifunzaji wa lugha hujumuisha uamilifu wa matini. Kwamba, kuijua lugha kunahitaji kuwa na ufahamu wa kanuni za kijamii zinazotawala matumizi yake kama vile kanuni za kifonolojia, kisintaksia na za kisemantiki zinazomruhusu mtumiaji kuwasilisha mawazo au ujumbe wake (Kumaravadivelu, 2006). Kwa vile mawasiliano yanahusu mzungumzaji na hadhira, uamilifu wa lugha utawezeshwa vema kwa kuzingatia sifa za kiisimujamii zinazosababisha kuwepo kwa uhusiano na majukumu ya kutekelezwa kupitia kwa lugha. Sifa hizi za kiisimujamii huchangia kupatikana kwa maana iliyokusudiwa na mzungumzaji.
Austin naye anachukulia lugha kuwa uzungumzaji unaoshirikisha vitendo. Lugha ni mfululizo wa vitendo vinavyoambatana na maneno na wala sio mkusanyo wa istilahi na msamiati. Baadhi ya vitendo vinavyotimizwa na lugha ni kuamkuana, kuamuru, kufafanua, kukubali, kufahamisha, kuonya na kushangaa. Hata hivyo, maana ya kitendo husika itafahamika tu wakati kitendo hicho kinapotiwa kwenye muktadha wa kimawasiliano. Mtaala mpya wa Kiswahili umesistiza ufundishaji lugha kwa njia ya kuimarisha mawasiliano ya mwanafunzi ndani na nje ya darasa. Ili kumwezesha mwanafunzi kushiriki kwenye mazungumzo, mijadala, usomaji na uhakiki wa kazi za fasihi, mwelekeo wa kimawasiliano unafaa zaidi kutumika kwa ujifunzaji. Mwanafunzi asifunzwe tu vipengele vilivyojitenga kama vile sarufi, msamiati, masuala ibuka na fasihi, bali kila kipengele kichangie mazoezi ya kuwasiliana kikamilifu. Mawasiliano haya yafanywe kwa vitendo kama vile mwanafunzi mmoja kuomba msamaha kwa mwenzake, kumpa mwenzake ushauri, kuandaa na kuwasilisha hotuba darasani au kuwatangazia watu kuhusu bidhaa mpya.
Muhimu kwa mwanafunzi ni kupata nafasi ya kutagusana na kuchangiana maarifa wakati wa ujifunzaji (Omondi, Barasa, na Omulando, 2012).
Katika mwelekeo wa kimawasiliano, mwalimu wa Kiswahili anashauriwa kuzingatia yafuatayo:
- Matumizi ya Kiswahili katika mazingira halisi kama vile: mazungumzo mitaani, matangazo redioni, au mijadala bungeni. Miktadha ya kijamii huyapa mawasiliano maana kamilifu.
- Hadhira iweze kubaini waziwazi dhamira ya msemaji au mwandishi wa ujumbe unaowasilishwa.
- Dhana, hali au tukio moja linaweza kuelezwa kwa njia tofautitofauti au mitindo mbalimbali ya lugha. Vilevile, ujumbe mmoja unaweza kuwasilishwa kwa njia tofauti . Kwa mfano, mada ya uhakiki wa fasihi inaweza kuwasilishwa kupitia kwa insha, tangazo, wimbo au mchoro wa kisanii.
- Wanafunzi wahimizwe kupangua mfululizo wa sentensi katika matini, kuzitathmnini na kuzipanga upya kwa kuzingatia mbinu ya mwambatano na mshikamano. Lengo ni kumwezesha mwanafunzi kueleza ujumbe wa matini kwa maneno yake mwenyewe. Himizo na msaada wa mwalimu na wanafunzi wenza vinahitajika ili kumwezesha mwanafunzi kufikia upeo wa utendaji katika ujifunzaji wake wa lugha.
- Michezo ya lugha inaweza kutumika ili kunoa umaizi wa kimatamshi, wa kimisuli na wa kimazingira. Jukumu kubwa la mwalimu ni kuteua na kuwapa wanafunzi shughuli zinazochochea mawasiliano, huku akiwapa usaidizi uliokadiriwa.
- Wakati wanafunzi wanapowasiliana, makosa ya kisarufi yasitajwe moja kwa moja bali mwalimu ayanakili daftarini na kuyashughulikia baadaye.
(Larsen- Freeman, na Anderson, 2011)
Mwelekeo wa kimawasiliano unalenga kumshirikisha mwanafunzi katika ujifuzaji wa Kiswahili kwa kutumia shughuli zinazokuza aina tofauti za umaizi. Shughuli hizi humpa mwanafunzi nafasi ya kujieleza na kuthamini mawazo ya wengine katika mazingira anamoishi. Hata hivyo, mwelekeo huu utafana tu ikiwa tathmini na utahini wa stadi kama vile uandishi wa kiuamilifu, utunzi wa insha na uandishi wa kisanii utalenga zaidi uwezo wa mwanafunzi wa kujieleza kikamilifu.
- b) Mwelekeo wa Kimajukumu
Lengo la mwelekeo wa kimajukumu ni kumshirikisha mwanafunzi katika kutimiza majukumu yaliyo na matokeo yaliyotarajiwa. Jukumu la mwalimu ni kuandaa shughuli za ujifunzaji kutegemea mahitaji ya mwalimu. Mwanafunzi pia anahitaji kuandaliwa awali kabla ya kujaribu kutimiza majukumu ya kutumia lugha yaliyopangwa na mwalimu. Wakati wa utendaji mwalimu anahitajika kufanya tathmini ya mara kwa mara kwa kuchunguza na kuhimiza au kumrekebisha mwanafunzi, hatua kwa hatua hadi afikie kilele chake cha utendaji. Mwanafunzi hujifunza kutekeleza jukumu alilopewa kwa kushirikiana na wenzake, kupata usaidizi wa mwalimu na kupewa himizo hadi afikie kiwango kilicho bora cha matumizi ya lugha (Kumaravadivelu, 2006). Katika ufundishaji wa Kiswahili, jukumu teule lihusishwe na mojawapo ya masuala ibuka ili lishugulikiwe kama tatizo la kijamii.
Mtaala mpya unaainisha masuala ibuka katika vitengo vikuu vitano: uraia na uzalendo; afya na maradhi; stadi zamaisha na elimu ya kimaadili; elimu ya kukuza maendeleo endelevu na ushauri nasaha (Kenya Institute of Curriculum Development, 2017:110). Mwanafunzi anaweza kushirikishwa kutafuta suhuhisho kuhusu masuala kama vile jinsi ya kutunza na kulinda maslahi ya watoto; namna ya kukabliana na maradhi yanayotokana na mikondo ya maisha ya watu; au jinsi ya kukuza jamii yenye ufahamu kuhusu mbinu za uzalishaji mali. Masuala haya yanafaa kumshughulisha kila mshika dau kwenye mfumo wa elimu ili kupata suluhisho la kudumu.
Kwa mujibu wa Ellis (Ellis, 2007) kuna aina tano za majukumu yanayoweza kupangiwa wanafunzi katika somo la lugha. Nayo ni:
- Jukumu linalohitaji ubadilishanaji wa maarifa ili kujaza pengo. Kwa mfano, katika somo la insha, mwanafunzzi mmoja asimulie kuhusu tukio fulani kama vile uwindaji haramu huku mwenzake akichora picha kulisawiri tukio hilo daftarini. Kisha waandike insha kuhusu jinsi ya kukomesha visa vya uwindaji haramu wa wanyama pori.
- Masuala ibuka mengi hutokea kama tatizo kwa jamii. Wanafunzi wanaweza kupewa jukumu la kutoa maoni yao kuhusu suala nyeti kama vile jinsi ya kuzuia vijana wasijiunge na makundi yanayotekeleza ugaidi wa kimatifa. Baada ya kujadili na kutoa maoni yao wanafunzi wanaweza kuandika barua ya kumpa mwenzao mawaidha kuhusu athari za kushirikiana na ugaidi wa kimataifa na kupendekeza jinsi ya kudumisha uzalendo na mlahaka mwema katika jamii.
- Wakati mwingine, mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi hali na taarifa fulani itakayowahitaji kutafakari ili kupata suluhisho. Jukumu la mwanafunzi litakuwa ni kufikiri kwa kwa makini ili kutafuta utatuzi. Kwa mfano, mwanafunzi atafakari jinsi atakavyomsaidia mgeni aliyetua kwa uwanja wa ndege, na asiyeifahamu lugha yake, namna atakavyofikia kituo cha mabasi ili kusafiri hadi hotelini jijini. Huenda mwanafunzi huyo akamchorea ramani, au akatumia lugha ishara au akatumia picha kuwasiliana na mgeni yule au akaamua kuandamana naye mwenyewe hadi hotelini.
- Mwalimu pia anaweza kuteuwa majukumu yasiyobainika waziwazi. Haya ni najukumu ya kubuni yanayomhitaji mwanafunzi kufikiri na kujifaragua. Kwa mfano, mwalimu wa Kiswahili anaweza kuwapa wanafunzi kupanga ziara ya kubuni ya kuzuru pwani mwa Kenya kwa kutumia gari moshi. Jukumu hili litawahitaji wanafunzi kujadiliana, kuandaa mipangilio ya safari, kuigiza baadhi ya hatua za ziara, kuandaa vitambulisho vya mikoba, kusakura mitandao ili kubaini maeneo bora ya kuzuru pamoja na gharama za malazi, huduma za mabasi ya umma na mengine mengi. Kisha kila kikundi kipewe nafasi kuwasilisha majibu yao ili yachangiwe na kuimarishwa.
- Pia majukumu maalum yanayolenga wanafunzi kuwasiliana kwa sajili fulani yanaweza kutumika kufunza Kiswahili. Tatizo linaweza kuwahitaji wanafunzi kuonyesha jinsi ya kuwaokoa waathiriwa wa mkasa wa mafuriko. Wanafunzi watahitajika kuwa na ufahamu wa kutoa huduma ya kwanza, mbinu za kuwasiliana kwa dharura na waokoaji, lugha ya hospitali na jinsi ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Jukumu hili litahitaji utendaji wa dharura lakini ulio na mpangilio maalum. Pia, wanafunzi watahitajika kutekeleza majukumu madogomadogo chini ya uongozi wa kinara wa shughuli hiyo. Jukumu hili huwezesha wanafunzi kusaidiana, kutegemeana na kujitahidi kwa pamoja ili kulitekeleza.
Kwa maoni ya Vygotsky (1978) mwanafunzi anaweza kufikia eneo la upeo wa ukuaji wake kwa kupewa majukumu yanayochochea tafakari ili kumpa motisha ya kutenda zaidi ya umri wake wa ukuaji. Mwalimu anahitajika kumudu mchakato mzima wa utelekezaji wa majukumu kwa kutoa uelekezi na himizo chanya kwa hatua za kusuluhisha tatizo lenyewe. Dhima ya himizo chanya na usaidizi kutoka kwa mwalimu au wanafunzi wenza ni: kumfanya mwanafunzi ajiamini; kumpa matumani kuwa anaweza kutimiza jukumu; kumpa kuridhika anapotekeleza jukumu kwa ufanisi na kuchochea mashindano ya utendaji miongoni mwa wanafunzi (Dweck, 2000). Mwanafunzi anapohimizwa anaweza kutekeleza majukumu makubwa hata kuliko umri wake wa ukuaji. Mtaala mpya wa elimu unalenga kumpa mwanafunzi matumizi ya lugha ili kumwezesha kukuza: tafakari za umakinifu, ubunifu, ufaraguzi, kujiamini na kutumia nyenzo za kidijitali kupata maarifa. Mwelekeo unaoweza kuchangia zaidi utekelezwaji wa malengo haya pamoja na kuhimiza ujifunzaji usio na kikomo ni mwelekeo mseto, unaojumuisha mielekeo ya kimawasiliano na kimajukumu.
- Mwelekeo Mseto
Huu ni mwelekeo unaohimiza ujifunzaji wa stadi, vipengele vya lugha na tanzu za fasihi kwa pamoja ili kuimarishana na kumwezesha mwanafunzi kufahamu Kiswahili kama somo moja lisilo na vitengo. Chan (2005) anautaja mtaala unaozingatia mwelekeo mseto kuwa wenye vipengele vifautavyo:
- Uhusisho wa dhana mpya na maarifa ya awali aliyo nayo mwanafunzi kwa lengo la kukuza mshikamano wa maarifa hayo akilini.
- Maarifa anayojifunza mwanafunzi yawe ya kumfaa katika hali halisi ya maisha. Mifano ya kuelezea dhana za lugha itoke kwenye mandhari ya mwanafunzi.
- Mtaala ulenge kuimarisha mbinu za utatuzi wa mambo ili kupunguza hali ya kuwepo kwa wanafunzi waliopita mitihani vema lakini wasioweza kuhamisha maarifa yao kutatua matatizo katika jamii.
- Msisitizo uwe kwenye matumizi ya sayansi na teknolojia ili kuwezesha ujifunzaji wa kidijitali unaomwezesha mwanafunzi kuelewa upeo na ufinyu wa sayansi katika kusuluhisha matatizo ya kijamii.
Katika ujifunzaji wa Kiswahili, mwelekeo mseto unapendekeza kutumia matini kutoka kwa masomo na taaluma tofautitofauti kuzua tatizo la kushughulikiwa na wanafunzi. Kwa mfano, kutumia makala ya haki za watoto kutoka kwa somo la Historia ili kujadili namna ya kukomesha unnyanyapaa unaofanyiwa mayatima. Mwelekeo mseto unawezeshwa kupitia kwa nadharia ya ujifunzaji wa vitendo, mitagusano ya kijamii, umaizi mseto na ujifunzaji unaaonekana. Nabors (2012)anapendekeza walimu kutumia mikakati shirikishi kama: vile utatuzi wa mambo, uhusisho wa dhana akilini, dayolojia na vikundi. Mikakati hii humhitaji mwanafunzi kushiriki ujifunzaji kupitia hisia, utendaji, tafakari na kushirikiana na wenzake ili kujijengea maarifa ya kumsaidia kuishi katika jamii.
Mikakati Shirikishi ya Kufunzia Kiswahili
- Ujifunzaji wa Kuongozwa
Huu ni mfululizo wa mafunzo yanayotolewa katika vikundi vidogo vya wanafunzi wakati wa kipindi cha kawaida cha somo. Mkakati huu humwezesha mwalimu kufunza darasa zima huku akihimiza shughuli za kibinafsi kwa kila mwanafunzi kwa wakati mmoja (Department for Education and Skills, 2004). Katika ufundishaji wa kuogozwa, mwalimu hufunza moja kwa moja ili kumpa kila mwanafunzi fursa ya kubwia na kujiundia dhana au stadi maalum katika somo. Aghalabu, vipindi vya ufundishaji wa kuongozwa huchukuwa muda kati ya dakika 10-30, kutegemea ugumu wa shughuli au stadi inayofunzwa. Jambo muhimu kwa ujifunzaji wa kuongozwa ni kuwa mwanafunzi hutawala shughuli ya ujifunzaji kwa kuelekezwa kupitia kwa kikundi.
Mwalimu huteuwa shughuli za ujifunzaji na kuziratibu kwa makini ili zimpe mwanafunzi kichocheo cha kutafuta suluhisho. Kikundi huwezesha ushirikiano na kuchangiana maarifa. Mkakati wa mwalimu ni kumuimarisha mwanafunzi kupitia kwa msaada ulioratibiwa ili aweze kujitegemea binafsi katika kushughulikia jukumu alilopangiwa. Uimarisho huu, kwa mujibu wa Vygotsky, unaweza kufanywa kwa hatua kama vile: anapoandika, anaposoma, anapozungumza, anapopanga hoja za utungaji wa insha, au anapofanya zoezi. Shughuli za ujifunzaji hupangwa kwa kuzingatia mahitaji na udhaifu wa wanafunzi kwenye kikundi. Mwalimu huwapa usaidizi ili kuwahimiza kwa viwango hadi watakapoweza kutekeleza jukumu lao wenyewe. Pia, kujitegemea kwa wanafunzi katika utendaji kunaweza kutokana na msaada wa wanafunzi wenza, utafiti, mitagusano na ushirikiano katika shughuli za ujifunzaji.
Kwa mujibu wa Roehler na Cantlon (1997) mwalimu anaweza kuwaimarisha wanafunzi kwa mikakati ifuatayo:
- Kuwapa ufafanuzi wa dhana kama vile kufafanua dhana ya utandawazi kisha kuwauliza wanafunzi kutaja nyenzo zinazowezesha usambazwaji wa habari, matukio na maarifa ulimwenguni. Mwalimu anaweza kutumia majibu ya mwanafunzi kufafanua dhana zaidi ili kuifanya ieleweke vizuri. Baada ya kufafanua dhana kuu ya somo, wanafunzi huachiwa dhana nyingine ili wajifafanulie wenyewe kwenye kikundi.
- Kuwaalika wanafunzi kutoa maoni yao kuhusu somo. Kwa mfano, katika somo linalohusu athari za utandawazi kwa maadili ya vijana, mwalimu anaweza kuwaalika wanafunzi kutoa maoni yao kuhusu vyombo vya habari hasa magazeti, kanda za video, mitandao na rununu. Mwanafunzi asimulie tajiriba yake na vyombo vya mawasiliano. Baada ya wanafunzi watatu kuchangia maelezo yao, mwalimu aondoe mkakati huu na kuwapa majukumu ya vikundi ili wajadili athari chanya na hasi za chombo kimoja cha mawasiliano kwa kila kikundi.
- Mwalimu akadirie majibu na weledi wa mwanafunzi kuhusu hoja anazozitoa kwenye vikundi. Majibu yaliyo sahihi na yenye kutolewa ithibati na wanakikundi yahimizwe na kutuzwa na mwalimu. Majibu yasiyo sahihi yarekebishwe na mwalimu huku akisistiza kutolewa kwa ithibati. Kisha wanafunzi wapewe fursa ya kujitafutia hoja zenye ithibati wenyewe wakiwa vikundini.
- Mwalimu aongoze wanafunzi kufikiri kwa kutamka kile wanachokifikiri kuhusu jukumu walilopangiwa kutimiza. Maswali ya kuchochea fikra za mwanafunzi yanaweza kutumiwa na mwalimu. Kwa mfano, katika kushughulikia jukumu linalohitaji wanafunzi kupendekeza namna ya kumaliza uuzwaji na unywaji wa pombe haramu, mwalimu atamke fikra zake kwanza, kisha awahimize wanafunzi kuzichangia. Mawazo yao yanukuliwe ubaoni na kutathminiwa na wenzao kwenye kikundi.
Katika kutoa himizo kwa kikundi, mwalimu atuze juhudi zinazoelekea zaidi kutoa suluhisho kwa tatizo. Mwalimu anaweza kuwapa wanafunzi zoezi la kutathmini utendaji wao katika kikundi. Zoezi lilenge uhamishaji wa maarifa kutoka kwa muktadha mmoja hadi mwingine. Kwa mfano, somo la mjadala kuhusu namna ya kumaliza pombe haramu linaweza kutathminiwa kwa wanafunzi kuandika barua ya mapendekezo kwa Gavana wa Kaunti au kutunga mchezo wa kuigiza wa kuhamasisha umma. Katika ujifunzaji wa Kiswahili, mwalimu anashauriwa kuwa mwelekezi tu, bali wanafunzi wenyewe wahimizwe kufikia suluhisho la tatizo au jukumu walilopewa.
- b) Kazi Mradi
Ni mbinu inayowezesha ujifunzaji kwa njia ya kuchunguza maumbile, kutagusana kijamii, kushiriki kwa vikundi na kuchangiana maarifa yanayotokana na aina tofauti ya umaizi wa wanafunzi. Njia hii ilipendekezwa na Montessori (1870-1952), Pestalozzi (1746-1827) na Vygotsky (1896-1934); miongoni mwa wanasaikolojia wengine. Mikakati inayotumika katika mbinu hii ni michezo na kutangamana baina ya wanafunzi ili kupanua tajiriba. Kulingana na Vygotsky (1978) mbinu ya kazi mradi hutambua maarifa ya awali ya mwanafunzi kama wenzo mkuu wa ujifunzaji wa maarifa mapya. Katika ujifunzaji wa Kiswahili, maarifa ya awali yanaweza kuwa ni umilisi wa lugha ya kwanza ya mtoto, ambao unaweza kutumika kumwelekeza kujifunza Kiswahili kama lugha ya pili.
Kazi mradi hushirikisha upataji wa maarifa na stadi mseto kwa pamoja kama vile: Hisabati, kusoma, kujadiliana, kuandika, mafunzo ya kijamii, Sayansi na udadisi. Katika Kiswahili, wanafunzi wanaweza kupewa kazi mradi ya kutafitia majina ya mimea iliyomo kwenye mazingira ya shule, ili kujifunza kuhusu nomino za pekee. Ili kutimiza shughuli hii, watajigawa kwenye vikundi kushughulikia: miti ya matunda; mimea ya nafaka; nyasi; mboga za kienyeji; mimea ya kurembesha mazingira; na mimea inayoliwa na binadamu. Shughuli za ujifunzaji zitawahitaji wanakikundi:
- Kuzuru eneo la shule kama vile vitalu, ua, shamba au vichaka.
- Kuchora ramani ya shule yao.
- Kupiga picha za baadhi ya mimea na kuzibandika kwenye ripoti yao.
- Kujadiliana kuhusu muundo wa ripoti ya kikundi.
- Kutafsiri majina ya mimea kwa Kiswahili sanifu.
- Kutunga shairi kuhusu umuhimu wa mimea waliyotafitia.
- Kuwasilisha ripoti yao.
- Kuandaa makala maalum kuhusu majina ya mimea kwa Kiswahili ili yachapishwe kwenye gazeti la shule au yaangikwe kwenye ubao wa matangazo wa shule.
Mradi huu utawahitaji wanafunzi kutafuta utaalamu wa tafsiri, uchoraji wa ramani, upigaji picha, na ufahamu wa masomo ya Kilimo na Bayolojia. Uimarisho wa mwalimu ni muhimu katika kuwahimiza na kuwasaidia wanafunzi kufafanua dhana. Kazi mradi huwapa wanafunzi fursa ya kubadilishana maarifa, kushirikiana na kupanua tajiriba zao. Shughuli za vikundi kwenye kazi mradi zinafaa kushirikisha wanafunzi wenye aina tofauti za umaizi ili washirikiane kupanga mikakati ya utekelezwaji, ugavi wa majukumu, ukusanyaji wa data, kupanga matokeo na kuyawasilisha darasani. Kikundi kinachowasilisha kazi bora zaidi kinastahili kutuzwa na mwalimu ili kuhimiza ushindani baina ya wanafunzi.
Udhaifu wa Nadharia ya Umaizi Mseto katika Ufundishaji wa Kiswahili
Ingawa lengo kuu la mtaala mpya ni kutimiza Malengo Endelevu kwa kuegemeza ufundishaji kwenye nadharia ya bunilizi, utekezwaji wa ruwaza ya mabadiliko ya kielimu nchini Kenya unatarajiwa kukumbwa na changamoto. Ufundishaji wa masomo ya Lugha na Fasihi ya Kiswahili utakumbwa na changamoto zifuatazo:
- Uhaba wa walimu walio na ufahamu na tajiriba ya kutosha kutelekeza nadharia ya umaizi mseto. Tajiriba waliyo nayo walimu wengi wa Kiswahili ni kufunza somo kwa kuwapa wanafunzi mazoezi ya kuwakaririsha dhana ili wapite mitihani ya kitaifa. Ili kufaulisha uimarishwaji wa vipawa katika somo la Kiswahili, ipo haja ya kuunda upya mikakati ya kutathmini utendaji wa mwanafunzi.
- Muda wa kufunza masomo kwa kunawirisha aina tofauti za umaizi huenda ukawa kikwazo. Mada zilizoorodheshwa kwenye mtaala wa Kiswahili zinahusu mbinu za mawasiliano, sarufi, kusoma, kuhakiki, kuigiza na kutafitia tanzu za fasihi. Mwanafunzi anatakiwa pia ashiriki kwenye mijadala kuhusu masuala ibuka, kushiriki kwenye tamasha za sanaa za maigizo na kuchangia midahalo kuhusu tahakiki za vitabu teule. Mtaala hauonyeshi mfululizo wa mada wala mpangilio wa shughuli za ujifunzaji.
- Sera ya serikali ya kutoa elimu ya bure kwa shule za upili imechangia kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kwenye madarasa ilhali idadi ya walimu haiongezeki. Mwalimu anayedhamiria kufunza kwa umaizi mseto anahitaji muda mwingi wa kubaini vipawa vya kila mwanafunzi na mtindo wake wa ujifunzaji. Kuna uwezekano kuwa baadhi ya wanafunzi, hasa wale wanyamavu huenda wasipate nafasi ya kushughulikiwa na mwalimu katika mchakato wa ufundishaji.
- Gharama ya kumudu utekelezwaji wa umaizi mseto ni ghali. Ipo haja ya kutenga pesa za kununua nyenzo kama vile tarakilishi, kujenga maabara, vifaa vya michezo, nyenzo za uigizaji, ala za muziki pamoja na kuwaajiri wataalamu wa kutoa mafunzo hayo. Walimu waliopo hawajaandaliwa kufunza kwa mazingira yanayoruhusu ukuzaji wa vipawa.
- Lugha ya Kiswahili imepokelewa kwa mtazamo hasi kwa jamii ya Wakenya. Imani kwamba lugha za kigeni ni bora zaidi kutokana na uwezekano wa kupatikana kwa ajira za ujira mzuri huenda ikachangia wanafunzi wengi kutolichangamkia somo la Kiswahili. Pia desturi ya vijana wengi kupendelea kutumia lugha ya Sheng’ huenda ikaathiri idadi ya wanafunzi watakaoteua kujiendeleza kwa somo la Kiswahili. Wazazi wengi huenda wakawahimiza watoto wao kuegemea zaidi masomo ya Sayansi ya michezo kuliko sanaa.
Hitimisho
Katika makala hii, ufundishaji na ujifunzaji wa kwa misingi ya nadharia ya umaizi mseto umejadiliwa. Nadharia hii imependekezwa kwenye mtaala mpya wa elimu kama dira ya kulifikisha taifa kwa utekelezwaji wa Malengo Endelevu. Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unapendekeza kuwa elimu ichangie kutatua matatizo kama vile majanga ya njaa, ugonjwa na umaskini. Nadharia ya umaizi mseto inalenga kumshirikisha kila mwanafunzi kwa kukuza umaizi na vipawa vyake kwa kutambua na kutumia mikakati inayolenga mitindo mbalimbali ya ujifunzaji. Mitindo hii ya ujifunzaji imesukwa kwenye aina nane za umaizi, zinazonuia kukuza vipawa kama vile: ulumbi, muziki, michezo, uhandisi, falsafa, ujarabati, uhifadhi wa mazingira, sanaa na vingine vingi, ili kujenga jamii inayowatambua na kuwashirikisha watu wote katika maendeleo.
Nadharia ya umaizi mseto imefafanuliwa kwa misingi ya nadharia bunilizi zinazopendekezwa kuelekeza upataji wa maarifa. Baadhi ya nadharia hizi ni: mitagusano ya kijamii, ujifunzaji wa vitendo, ujifunzaji unaonekana, na nadharia ya ufundishaji wa lugha kimawasiliano. Msistizo ni kwa mwalimu kufunza Kiswahili kwa kutumia mbinu za umajukumu, vitendo, mawasiliano, utatuzi wa mambo na vikundi. Himizo chanya pamoja na usaidizi kwa mwanafunzi ili aweze kutekeleza majukumu aliyopangiwa kwa ukamilifu ni ngazi ya kumfikisha kwenye eneo la kilele ch ukuaji wake kielimu.
Mwalimu anashauriwa kumtambua kila mwanafunzi wake kuwa aliye na uwezo wa kuchakata maarifa, kujifunza kwa kuelekezwa vilivyo, na kuyahamisha maarifa aliyoyapata ili kutatua matatizo katika mazingira anamoishi. Ujifunzaji wa Kiswahili kwa mikakati shirikishi umwezeshe mwanafunzi kutafakari, kuunda uhusisho wa dhana na maarifa aliyo nayo, kukuza na kunawirisha vipawa vyake ili kumwandaa kwa ulimwengu wa kazi inayomfaa.
Marejeleo
Baraza la Kiswahili la Taifa. (2015). Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers Limited.
Chan, M. (2005). Features of an integrated primary curriculum. Redesigning pedagogy, research, policy and practice. Namyan Technological University.
Department for Education and Skills. (2004, March 18). Pedagogy and Practice: Teaching and learning in secondary schools- Leadership guide. Retrieved from www.dfes.gov.uk
Dweck, C. (2000). Self Theories: Their role in motivation, personality and development. Psychology Press.
East African Community. (2014). Draft Hamornized Curriculum structures and framework for the East African Community: Secondary Education. Arusha: East African Community.
Ellis, R. (2003). Task based language learning and teaching. Oxford: Oxford University Press.
Ellis, R. (2007). Task based language teaching: Sorting out the misunderstanding. International Journal of Applied Lingustics 19/3, 221-246.
Gardner, H. (1993). Multiple Intelligences: The theory into practice. New York: Basic Books.
Kenya Institute of Curriculum Development. (2017). Basic education curriculum framework: Nurturing every learner’s potential. Nairobi: Kenya Institute of Curriculum Development.
Koenig, R. (2009). K-8 Library design renovation: Accomodating multiple intelligences and learning styles. Florida: Florida State University.
Kumaravadivelu, B. (2006). Understanding language teaching: From method to post method. New Jersey: Erlbaum Associates Publishers.
Larsen- Freeman, D. & Anderson M. (2011). Techniques and principles in language teaching. New York: Oxford University Press.
Nabors, K. (2012). Active learning sytaregies in classroom teacching: Practices of associate degree nurse educators in a Southern State. University of Alabama.
Omondi, M.A., Barasa, P.L. & Omulando, C.A. (2012). Challenges teachers face in the use of Communicative language Teaching Approach in the teaching of listening and speaking lessons in Lugari District, Kenya. International Journal of Science and Research, 83-92.
Republic of Kenya. (2010). Summative Evaluation of the Secondary School Education Curriculum. Nairobi: Government Press.
Republic of Kenya. (2012). Session Paper No. 14 (2012): Reforming Education and Training in Kenya. Nairobi: Goverment Press.
Richards, J.C. & Schmidt, R. (2010). Longman dictionary of language teaching & applied lingistics (4th Ed.). Harlow: Pearson.
Roehler, L.S. & Cantlon, D.J. (1997). Scaffolding: A powerful tool in social constructivist classrooms. In K. &. Hogan K.& Pressley, M. (Eds.), Scaffolding student learning: Instructional approaches and issues. (pp. 6-42). Cambridge: Brookline Books.
United Nations. (2016). The Sustainabe Development Goals report. (pp. 2-5). New York: United Nations.
Vygostky, L. (1978). Interaction between learning and development. Readings on the development of children, 34-40.
Zhou, M. &. (2014). Educational Learning Theories. Retrieved March 17, 2018, from http://creativecommons.org