Tathmini Ya Ujumi Mweusi Katika Tamthilia Ya Mashetani Wamerudi (S.A.M 2016)
Justus Kyalo Muusya
Chuo Kikuu cha Kenyatta
Barua pepe:muusyaj@yahoo.co
Ikisiri
Tamthilia ya Kiswahili ina historia fupi ikilinganishwa na tanzu zingine, hasa ushairi. Tamthilia za kwanza kuwahi kutafsiriwa kwa Kiswahili na zilizoandikwa kwa lugha hii zilizingatia sana maudhui ya kidini, kizalendo, utetezi dhidi ya dhuluma tawala za kigeni na hasa ukoloni mamboleo. Kinyume na hali hiyo, tamthilia ya Kiswahili katika kipindi cha kuanzia 1950 hadi miaka ya 2000 umesheheni wingi wa tungo zinazosifia Uafrika na heshima ya mtu mweusi hapa barani Afrika na kote ulimwenguni. Uchunguzi wa tamthilia hizi unadhihirisha kujitolea kwa dhati kwa watunzi wake kuelezea, kutetea na kuhimiza heshima ya Mwafrika. Maudhui yake yanakiuka yale masuala finyu ya utaifa, uraia na tawala za mataifa ya Kiafrika. Hii ndio maana makala haya yanalenga kufafanua nadharia na maoni ya wanaujumi mweusi na jinsi fikira zao zilivyoathiri na kuongoza mitazamo ya watunzi wa tamthilia. Data ya makala haya ilikusanywa katika tamthilia ya Mashetani Wamerudi (Mohamed 2016). Tamthilia hii iliteuliwa kwa kutumia mbinu kusudio. Hii ni kwa sababu usomi awali ulionyesha kuwa tamthilia hii imetumia misingi ya nadharia ya ujumi mweusi. Data yenyewe ilikuwa ya kimaelezo na ilichanganuliwa vilevile kwa njia ya maelezo. Makala yalionyesha namna ambavyo mwandishi ameweka wazi hadhi ya Mwafrika na kudhihirisha kuwa amejitambua na anapaswa kutambuliwa na kuheshimiwa na ulimwengu mzima. Hii ni baada ya Mwafrika kuelewa kwamba watu kutoka mabara mengine sio bora kumliko kama ambavyo watu hawa hutaka ichukuliwe na Mwafrika.
Istilahi Muhimu: ujumi mweusi, uafrika, ukoloni mamboleo, utandawazi, wakoloni na utaifa
Misingi ya nadharia
Kwa mujibu wa Zirimu (1971), ujumi ni vigezo vinavyotumiwa kuainisha urembo wa sanaa. Kila jamii huwa na vigezo vyake maalum vya aina hii. Vigezo hivi ndivyo hutumiwa kuainisha sanaa katika jamii husika. Zirimu anaongeza kuwa, wasomi ambao wanatumia vigezo vya kigeni kuainisha fasihi za kiafrika sio wahakiki bora kwa vile wanaiga tu mambo ya kwingineko. Kwa sababu hii, anapendekeza uhakiki bora wa fasihi ya Kiafrika ni ule unaotokana na jamii yenyewe ya Kiafrika. Hivyo, ujumi mweusi unapaswa kutokana na mazingira ya watu weusi.
Kulingana na Wafula na Njogu (2007), ujumi mweusi ni zao na jaribio la Mwafrika la kushughulikia wema wa utamaduni wake pamoja na kuelewa historia yake. Hii ni kwa sababu Mwafrika amekuwa akibaguliwa na kudhalilishwa kila anapouhusiana na kuingiliana na wageni kutoka nje ya bara la Afrika.
Falsafa za kimagharibi zimekuwa wazi kuhusu uduni na ulaanifu wa Mwafrika tangu kuumbwa kwake. Kwamba, huwezi kutarajia ustaarabu wa aina yoyote kutokana na kiumbe cha aina hii. Akisisitiza kauli hii, Hume, kama alivyonukuliwa na Curtin (1964) anaeleza kuwa Waafrika ni wajinga kwa sababu wazazi wao wa mwanzo walikuwa wajinga. Mawazo haya ndiyo yaliyopalilia na kukuza falsafa ya kikoloni na utumwa. Ikamfanya mtu mweupe kumchukulia Mwafrika kuwa mtumwa wake kwa karne nyingi.
Hivyo, mkoloni alifikiri kwamba Mwafrika hangezingatia mbinu za usanii wa fasihi. Maoni ya wakoloni kama haya ndiyo yamemsukuma Mwafrika kuutetea utu wake, utamaduni wake na sanaa yake.
Ujumi mweusi kwa hivyo, umetokana na mazingira yaliyoshuhudia kukandamizwa kwa Mwafrika katika Nyanja zote za maisha. Ulizuka kama upinzani dhidi ya hujuma zilizofanywa na wakoloni dhidi ya heshima yake. Hujuma hizi ni pamoja na hali ambapo rangi nyeusi, rangi ya Mwafrika inachukuliwa na Wanamagharibi kuwa ishara ya mauti na kuzimu au ishara ya makazi ya shetani.
Katika juhudi za kutetea heshima ya Mwafrika, Waafrika wameweza kuunda istilahi zinazoonyesha ustaarabu, fahari na wema wa Uafrika. Istilahi hizi ni pamoja na: Wamerikani Weusi, Waislamu Weusi, Nguvu Nyeusi na zingine (Wafula na Njogu 2007). Kwa kufanya hivyo, wamedhihirisha kwamba Mwafrika anauonea fahari utu wake, rangi yake na hata matendo yake. Hii ndio maana Senghor anaeleza ujumi mweusi kama jumla ya ustaarabu na mapokezi mengine yanayothaminiwa na ulimwengu wa Kiafrika.
Hata hivyo, ni muhimu kutaja kuwa Mwafrika mwenyewe amekubali kwa hiari yake kujiweka chini ya himaya ya wakoloni kwa njia mbalimbali. Kwa mfano, wasomi wameamini kuwa kila chema kinatoka kwa wakoloni. Hivyo wakaiga moja kwa moja. Dini vilevile imeshadidia ushenzi na giza iliyokuwapo Afrika kabla ya majilio ya Wamishenari.
Katika harakati za kutetea Mwafrika, Senghor aliyachukua mambo yale yaliyotumiwa na Wazungu kuwakashfu Waafrika na kuyapa maana ya heshima na taadhima kuu. Anatumia lugha ya hadhi.
Naye Cesaire (1968) anachukulia kuwa vita vya wanaoteswa dhidi ya watesaji wao ni mithili ya mashua inayoelea kwenye bahari ya mawimbi mengi. Anaamini kuwa, pamoja na udhaifu na uchochole wa wadhulumiwa, ushindi na haki viko upande wao.
Katika nadharia hii, tunabaini kuwa, falsafa zilizokuwa zikitumiwa na Wazungu kuwatawala Waafrika zilikuwa na uongo. Ni nadharia ambayo inatambua matumizi ya lugha za Kiafrika kwa mapana, na kwamba pale ambapo lugha ya Kiingereza itatumika katika kuiandika fasihi ya Kiafrika, inapaswa kufinyangwa na kufungamanishwa na ujumi wa Kiafrika.
Kunayo matapo kadha kuhusu ujumi mweusi. Ipo vilevile mihimili chungu nzima ya nadharia hii ya ujumi mweusi. Kati ya mihimili muhimu ni matumizi ya nyimbo zinazousifu Uafrika na kutilia mkazo usawa wa watu wote, weupe kwa weusi. Hata hivyo, mihimili ambayo imeongoza uhakiki katika makala haya ni ile ambayo iliongezewa na Asante Molefi (1999). Mihimili ambayo ilichangiwa na Molefi ni kama ifuatavyo:
Kumtibu mtu mweusi kutokana na matatizo ya kisaikolojia yaliyotokana na athari za ukoloni pamoja na kudunishwa.
Kuboresha nafasi ya mtu mweusi kisiasa, kijamii, kiuchumi na kidini.
Kudhihirisha kuwa mtu mweusi ndiye msingi wa ustaarabu wote ulimwenguni.
Utangulizi
Tamthilia ya Mashetani Wamerudi (2016) imeandikwa na Said Mohamed. Mohamed ni mwandishi mashuhuri wa fani zote za fasihi zikiwepo riwaya, tamthilia, diwani za hadithi fupi na za mashairi. Lakini ametumia upekee wa aina fulani katika tamthlia hii. Anwani Mashetani Wamerudi ameikuza kutokana na anwani ya Mashetani (Hussein 1971). Katika tamthilia ya Hussein, tunaona hafla ambapo shetani na binadamu wanacheza na kufurahia ili kuagana kwaheri. Hapa, shetani ni mkoloni na binadamu ni Mwafrika. Kuagana maana yake ni kuondoka kwa mkoloni huku Mwafrika akijipatia uhuru wa bendera. Hii ina maana kuwa hafla hii ilikuwa ni sherehe za uhuru wa Mwafrika.
Kwa misingi hii basi, Mohamed anataka tuamini kuwa ikiwa kweli wakoloni waliondoka kutoka bara la Afrika kufikia mwisho wa ukoloni mkongwe, basi wameweza kurudi kwa taswira tofauti. Kwamba wameweza kurudi kwa taswira ya ukoloni mamboleo katika miaka ya punde baada ya uhuru wa bendera, na kwa mtindo wa utandawazi katika siku za hivi karibuni.
Suala hili la utandawazi lilimchochea sana Mohamed katika kuandika tamthlia hii. Anadokeza kuwa alitarajia kwamba Hussein angeandika tamthilia nyingine baada ya Mashetani kuendeleza usawiri wa unyonywaji wa bara la Afrika na watu wa mabara mengine kupitia utandawazi. Alipoona amelimatia kufanya hivyo, akajitosa katika kuendeleza masimulizi alipoachia Hussein. Kwenye dibaji ya Mashetani Wamerudi, Mohamed mwenyewe anasema hivi:
… mpaka sasa, hajaandika au hajatoa tamthilia inayogonga kwenye usasa mpya wa ‘utandawazi’, ambao ni mfumo wa dunia wenye mchanganyiko wa siasa, uchumi, usafiri, biashara, uhaulishaji wa fedha kwa kasi, uanahabari, ugenini, ukimbizi wa makundi kwa makundi ya watu kuelekea nchi za ng’ambo (2016:iv)
Ni kana kuwa mwandishi wa Mashetani Wamerudi anaendeleza masimulizi na historia ya jamii ya Kiafrika, kisiasa kutoka pale ambapo Hussein alikomea katika Mashetani. Haya yanadhihirika bayana kwa njia tofauti. Katika tamthilia ya Hussein, wahusika wakuu ni Juma na Kitaru. Juma alikuwa anawakilisha wakoloni naye Kitaru akawa anawakilisha Waafrika. Hawa walikuwa ni wanafunzi wa chuo kikuu. Inaonekana kuwa naye Mohamed anawafinyanga wahusika wake wawili kutokana na hawa. Hawa ni Mzee Jumai na Mzee Kitarua. Ni kana kuwa anatuambia kuwa hawa waliokuwa vijana mapema miaka ya sabini wamekwishakuwa wazee. Kukomaa huku kwao kunawafanya hata mawazo, falsafa na matendo kubadilika. Zaidi ni kuwa, Juma na Kitaru walikuwa na mchezo wao. Mchezo wa mashetani. Kutokana na mchezo huu, Mohamed amebuni mhusika anayemwita Shetani au kwa kifupi Sheta.
Athari za ukoloni kwa Waafrika
Nadharia ya ujumi mweusi ilinuia kumponya mtu mweusi kutokana na athari alizopata kutokana na ukoloni mkongwe na baadaye ukoloni mambo leo. Athari hizi zilikuwa za kisaikolojia, kitamaduni na kilugha. Ilinuia vilevile kumponya kutokana na aina yoyote ya udunishwaji na watu kutokana nje ya bara la Afrika.
Wakoloni walitufanya tuamini kuwa chochote chenye asili ya Kiafrika ni kibaya na kiovu. Hivyo, kilicho chema kinatokana na Mzungu. Jambo hili lilipelekea Mwafrika kujichukia na kuchukia kila alichokuwa nacho. Lakini tunaona Prof. akiongoza katika kumzindua Mwafrika kutokana na hali hii. Anaonyesha kuwa baadhi ya vitu walivyokuwa navyo Waafrika ni bora kuliko vingine vya Wazungu. Anakunywa togwa ya kiasili (uk. 3). Anaeleza kuwa togwa ilikuwa tamu na bora kwa mwili wa mtu kuliko Coca Cola. Anasema hivi:
Aaaaa, togwa tamu hii. Tamu tokea kinywani mpaka damuni. Coca Cola itawezaje kutia fora mbele ya togwa?… kibaya kiwe chetu daima na kizuri kiwe chao daima. Kibaya chao kiwe kizuri chetu! Coca Cola si kwa siha wala si kwa adha yoyote ikilinganishwa na togwa (uk. 7-8).
Mwandishi atamzindua Mwafrika apende na athamini alicho nacho na kuelewa kwamba sio kila kitokacho uzunguni huwa kizuri kwa Mwafrika.
Mwafrika ametambua kuwa mkoloni hakuondoka kama alivyodai. Kwamba Mwafrika hakuweza kupata uhuru kamili kama alivyotarajia. Ameweza kutambua kuwa alichopata ni uhuru wa bendera tu. Kijana 1 anauliza kama nchi yake iliweza kusonga mbele tangu sherehe zilipoandaliwa, Mwafrika na Mzungu wakacheza wakisherehekea uhuru wa Mwafrika. Naye Prof. anamwambia kuwa mkoloni alirudi, na wala sio kama walivyodhani hapo awali. Prof. anaeleza namna hii:
Tokea shetani alipojidai anaondoka tukadhani eti hatarudi? Kumbe alituchezea shere kwa mchezo wa maneno. Ndani ya miaka mingi ya dhuluma tumegundua kile tulichotiwa vichwani mwetu. Lakini kugundua hakutoshi (uk. 5).
Anaposema kuwa kugundua hakutoshi anaashiria kuwa Mwafrika anapotambua kuwa amenyanyasa na mkoloni katika kipindi cha ukoloni mkongwe na ukoloni mambo leo ni hatua muhimu kwa vile awali alidhani mkoloni alikuwa mshirika wake bora. Hata hivyo, ukweli ni kuwa mkoloni alikuwa anaangamiza watu na kukana matendo yao maovu, na kwamba analeta athari kubwa kwenye akili za Waafrika (uk. 12-13). Kwa sababu hii Mkoloni anapaswa kufurushwa kabisa (uk. 11).
Elimu ambayo mkoloni alimfundisha Mwafrika haikuwa na lengo la kumwendeleza Mwafrika. Badala yake ilikuwa na azima ya kumnufaisha mkoloni mwenyewe. Hata hivyo, mhusika Sheta anashangaa kuona kuwa elimu hiyo iliweza kumfaa Mwafrika kwa kiwango fulani, jambo ambalo halikudhamiriwa na mkoloni. Anamwambia Prof. hivi:
Aaa, bado unakumbuka tuliyoyatia vichwani mwenu? Tukayaficha kwa ubayakumbe mengine mazuri kwenu (uk. 17).
Baadaye Kijana 1 anamwambia Sheta kuwa wakoloni waliwamezesha Waafrika fikra mbovu katika uchumi, utamaduni na mwenendo wa kijamii katika mifumo ya elimu waliyowaletea (uk. 49). Hii ndio maana Kijana 4 anaweka wazi mfumo mbaya wa elimu katika nchi yake kwa kusema hivi:
Elimu hii tulirithi kutoka kwa wakoloni (uk. 58).
Hii ilijikita katika nadharia bila utendaji wowote. Hivyo ikawa haimpi msomi maarifa muhimu katika ujenzi wa taifa. Utambuzi huu unafaa kuendana na kubadilisha mfumo wa elimu katika mataifa ya Afrika ili kukithi mahitaji ya mataifa haya. Vilevile, mfumo huo wa elimu uliwapa Waafrika kiburi kiasi kuwa aliyesoma kuliko wenzake anawadharau sana. Anajiona kuwa bora kuwaliko. Hata hivyo, hali inabadilika. Prof. anafurahia hali ambapo vijana wanaanza mkutano bila ya kusubiri Prof. mwenyewe kuuanzisha rasmi (uk. 34). Vilevile Prof. alidhamini sana maoni na mchango wa vijana wa madaraja tofauti kielimu.
Tofauti na ilivyokuwa hapo awali, watu weusi wanajiamini. Wanajiona wanaoweza kushindana na Wazungu na wakawashinda. Hili linadhihirika katika mazungumzo kati ya Sheta na Prof. namna hii;
Prof.: Na sisi tunajiamini pia.
Sheta: Mnajiamini?
Prof.: Ndiyo!…
Prof.: Basi hutanipiga kibao wakati huu. Labda utakapojitokeza.
Sheta: Nitakapojitokeza utakubali kupigwa kibao?
Prof.: Labda tupigane vibao.
Sheta: Utaweza?
Prof.: Hukunipiga zamani utanipiga kesho? (uk. 21).
Hapa inaonekana wazi kuwa Mwafrika alikuwa tayari kupigania uhuru, nafsi na haki yake. Suala hili linashangaza Wazungu kwa vile walikuwa hawajazoea ushindani wa aina hii kutoka kwa watu weusi.
Mtu mweusi anajaribu kupigana na sheria ambazo alitungiwa na kuletewa na Mzungu. Mojawapo ikiwa kwamba Prof. na wenzake watakuwa ni sharti wapate kibali cha polisi ili waweze kukutana kujadili mustakabali wao (uk. 25). Kwa Wazungu, sheria kama hizi zitalemaza juhudi zao za kujikomboa kwa vile hawatakuwa wanakutana kila mara watakavyo. Kuthibitisha kuwa walikuwa mbioni kujinasua kutokana na sheria hizi, Prof. anamjibu Sheta kama ifuatavyo:
Sheta: Kwa sababu sheria zetu lazima mzikubali na mzifuate. (Kwa ukavu).
Prof.: Sheria gani? (Kejeli).
Sheta: Kukusanya watu makundi kwa makundi lazima mpate kibali cha polisi.
Prof.: Polisi wanawalinda serikali au wananchi?
Sheta: Serikali ndiyo wananchi na wananchi ndio serikali.
Prof.: Ikiwa sheria ni hiyo, basi wananchi hawahitaji vibali vya polisi . Mkusanyiko wa watu usiokuwa na fujo ni haki ya wananchi na ni halali kabisa (uk. 25-26).
Aidha, suala la ushirikiano na umoja limepewa kipaombele katika kupambana na athari ya ukoloni. Hili ni muhimu kwa vile mkoloni alijaribu kila aliloweza kugawa Waafrika na kuwatawanya ili wasiungane kutetea uhuru na haki zao. Prof. anawahimiza vijana na wananchi kwa jumla washirikiane ili waweze kufaulu katika kupigania athari mbaya za ukoloni mongwe na ule wa mamboleo. Hii ndio maana kila walipokusanyika na kukaa pamoja, Prof. alikuwa anawasisitizia kukaa katika duara kama ishara ya kwamba wameshikamana kabisa. Anasema hivi:
Duara ni dunia Kijana. Duara linafinya. Linafumba. Lina taabu kupangua. Linashirikisha. Linalinda. Linafanya tutazamane. Kisha tushirikiane (uk. 30).
Hapa alikuwa anasisitiza umoja wa dhati uliokamilika. Huu ni umoja ambao haungevunjwa na wakoloni namna walivyozoea kuvunja hapo awali.
Kuboresha nafasi ya mtu mweusi
Nadharia ya ujumi mwesui hudhamiria vilevile kuimarisha nafasi ya mtu mweusi kisiasa, kijamii, kiuchumi na kidini. Mwandishi wa tamthilia ya Mashetani Wamerudi ameonyesha kuwa mtu mweusi ameweza kujipatia usemi kisiasa katika mahusiano yake na mkoloni. Hali hii ni tofauti na hapo awali. Mhusika Prof. anaeleza hali hii.
Mimi sijali Shetani anayepita au anayekita. Kama alipita jana Shetani ndiyo tulinyamaza. Lakini leo mwache apite. Sisi tutasema na matendo tutatenda! Tulisema wakati wa kutaka nchi yetu. Tutasema wakati huu wa baada ya kutawaliwa (uk. 4-5).
Baadaye tunaona mkoloni mwenyewe akikubali kuwa kuna mabadiliko katika mahusiano haya ingawa hakukuwa na usawa kamili. Sheta anasema namna hii:
Ukweli wa kwamba hatuko katika mfumo wa zamani wa unyonyaji wa ukoloni mamboleo (uk. 18).
Tunasoma kuwa wakoloni sasa walikuwa wameona haja ya kuwapa Waafrika msaada kidogo ili waendelee kiuchumi. Hata hivyo, kilichokuwa wazi ni kwamba wakoloni walinufaika zaidi kutoka kwa Waafrika kuliko msaada waliotoa.
Tatizo lingine ambalo watu weusi walikuwa sharti wakabiliane nalo ni uongozi wa Waafrika wenzao. Hii ni kwa sababu raslimali za watu weusi zikitwaliwa na wakoloni, natija ambayo inapaswa kuwaendea Waafrika kutokana na raslimali hizo huishia kwenye mifuko ya wachache. Hawa ni wale walio mamlakani na kuwaacha wananchi katika hali ya ukata. Hivyo, viongozi kama hawa wanashirikiana na wakoloni kuwadhulumu wananchi haki yao. Uongozi huu ni sehemu ya ukoloni mamboleo ambayo sharti ifurushwe ili kuwepo na usawa kamili. Sheta anashangaa ni kwa nini Prof. haigi tabia hii kwa manufaa ya kibinafsi. Anasema hivi:
… wewe peke yako ndiye unayekataa ukweli wa maisha mazuri yatayotazamiwa karibuni (uk. 19).
Baadaye Prof. anamjibu hivi:
Hizo pesa mnazotupa ni tone la asali analofyonza chozi. Kisha kasma kubwa zinaliwa na wakubwa. (uk. 19).
Angaa hii ni hatua murua kwamba Mwafrika amepata sauti ya kusimama kidete na kusema ukweli mchungu kwa wakoloni na washirika wao Waafrika.
Kwa kinywa kipana Mwafrika anasema kuwa yeye na Mzungu wanafaa kuwa sawa katika biashara na maingiliano mengine ya kiuchumi. Hivi kwamba, Mzungu asitoe kidogo kwa Mwafrika kwa kingi apatacho. Anashauri namna hii:
Bora tuheshimiane kwa haki za pande mbili. Lazima pande zote zipeane vipimo vya urari (uk. 20).
Wakati huohuo inawekwa bayana kwamba uchumi wenyewe wa nchi haujapiga hatua tangu uhuru. Masuala ya uchumi wa taifa yakawa yamevumbika giza kutokana na uongozi wa kikoloni mamboleo uliorithishwa kutoka kwa wakoloni. Hii ndio maana Kijana 3 anashauri kwamba ni bora taifa lijinasue kutokana na mkwamo huo wa kiuchumi. Kwa kufanya hivyo, litakoma kutegemea msaada na ufadhili kutoka kwa wakoloni. Hii ndio njia bora ya kukwepa athari za kikoloni katika mataifa huru. Hivi ndivyo Kijana 3 anavyosema:
Suala la kwenda mbele ni suala la kukataa kutegemea mapato kutoka nje kwa njia ya sadaka na ufadhili… ukweli ni kwamba wao (Wazungu) ndio wahitaji wakubwa wa raslimali na pia wahitaji wa kuuza bidhaa zao zinazotoka kwenye viwanda (uk. 57).
Baadaye Sheta anamwambia Kijana 1 kwamba upungufu ulioko nchini umesababishwa na viongozi wa nchi yenyewe, kwa hivyo si vyema kuwalaumu wakoloni kila mara (uk. 49). Naye kijana anasema,
‘Hao pia tutapigana nao mpaka watakapoanguka’.
Anachopigania hapa mwandishi ni uhuru wa kiuchumi. Anatambua kuwa tuna uwezo mkubwa wa kiuchumi, na kwamba tukiutumia vizuri tutakuwa wa kutegemewa na Wazungu kuliko vile tunavyowategemea.
Mfumo wa kisiasa wa mataifa ya Afrika ulirithishwa kutoka kwa Wazungu. Mfumo huu ulikuwa umebuniwa kwa lengo la kuwanufaisha wao na wala sio Waafrika. Waafrika wamepata usemi wa kuelekeza namna ambavyo utungaji wa sheria hizo na matumizi yake yanapaswa kuwa. Suala hili linajitokeza vyema katika majibizano kati ya Askari na wananchi. Angalia mfano huu:
Askari: … Wananchi… wananchi… wananchi. Simameni! Simameni! Maandamano haya si ya halali.
Kijana 1: (Kwa sauti kali na ya juu) Maandamano ya amani yasiyokuwa na fujo yana uhalali (uk. 75).
Kijana 3: Hatutaki sheria za mashetani.
Umma: Hatutaki… hatutaki… hatutaki sheria mbovu zinazomkuza shetani (uk. 75).
Kusuhu suala hilo la sheria naye Prof. anasema kuwa katika kutunga sheria bungeni, kusiwe na nguvu za chama tawala bali pia nguvu za upinzani. Hii ni kwa sababu kwa kushirikisha pande zote, wananchi watakuwa wameshirikishwa ipasavyo. Hata hivyo, Sheta anakataa kuamini uwezo wa Waafrika wa kujitungia sheria zozote kwa kusema hivi:
Nyinyi wanagenzi hamwezi kutunga sheria madhubuti (uk. 26).
Ili kuboresha uongozi na mahusiano ya kijamii, vijana wamepewa nafasi kubwa na usemi mkubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali. Awali ilikuwa kwamba ukweli ulikuwa ni milki ya wazee. Hivi kwamba, vijana walikuwa wa kuambiwa na wazee kile ambacho walidhani ndicho ukweli unaostahili. Hii ndio maana Prof. anatueleza hali hiyo namna hii:
Zamani ukweli ulikuwemo kichwani na kinywani mwa wazee na vijana waliwasikiliza na kufuata amri zao. Siku hizi vijana ndio walio na ukweli ambao wazee hawaukubali. Wanajua ukweli wa vijana ni ukweli thabiti kwa namna fulani! (uk. 35).
Kutokubali huku kwa vijana kunazua mvutano wa kitabaka, jambo ambalo linatinga mafanikio ya Mwafrika ya kuwa huru.
Mafaniko makubwa ya mwandishi wa tamthilia hii katika kukuza ujumi mweusi ni pale ambapo anaonyesha kuangamiza matabaka yaliyozuka katika jamii ya Kiafrika punde baada ya uhuru. Kulikuwapo na tabaka la mabwanyenye waliokuwa wamepoteza mamlaka na mali yao wakati wa mapinduzi. Nalo tabaka lililokuwa limepata mamlaka lilikuwa katika harakati za kujikusanyia mali nyingi kwa njia zisizo halali zaidi iwezekanavyo.
Kisha kulikuwapo na tabaka la chini la umma maskini. Hawa waliumia sana kwa kuongozwa vibaya katika mvutano wa matabaka haya mawili. Mzee Jumai anasema kuwa wakati umefika wa kuongea wazi na kinaganaga. Ndipo Mzee Kitarua akamwambia hivi:
Mzee Kitarua: Aaa, nilifundishwa na fikra za ushetani ili kwenda mbele kusikokuwa na mwisho: kunyonya, kubana, kukandamiza, kudhalilisha, kuchukua vitu vya watu, kulimbikiza, kuvunja sheria…
Mzee Jumai: Hayo yote si umesahau? Si unajua kwamba kabla ya nyinyi, sisi tulikuwepo katika kunyonya, kubana, kukandamiza, kudhalilisha, kuchukua vitu vya watu, kulimbikiza… (uk. 41-42)
Kijana 1 anasema athari za mvutano uliokuwapo wakati huo kwao ni …nchi yetu na sisi kuongozwa kama punguani au mabwege (uk. 62).
Kwa makundi haya kukubali tofauti zao na kuzizika, basi inamaanisha kuwa tumepiga hatua katika kufikia usawa kiuchumi na kujivua athari za ukoloni walizotuachia za kujigawa kimatabaka. Baadaye Mzee Jumai na Mzee Kitaru, ambao sasa wameishia kuwa marafiki wa dhati, wanaenda kumtembelea Prof. katika mazungumzo yao, wanamhakikishai kuwa walimaliza kabisa mfarakano uliokuwapo baina yao kwa sababu ya tajriba waliokuwa wamepata. Tajriba hiyo iliwafungua macho wakatambua ukweli (uk. 64-5).
Waafrika wanatambua pia kwamba namna mpya ambayo kwayo Mzungu anamtawala Mwafrika ni kupitia utandawazi. Utandawazi unachukua nafasi ya ukoloni mambo leo. Tofauti na ilivyokuwa awali, Mwafrika anauelewa ujanja huu wa kubadilisha mbinu kuendeleza maslahi ya awali. Tunabainisha haya katika majibizano kati ya Prof. na Sheta.
Sheta: … Kwani umesahau kwamba utandawazi ndio remote control zaidi kuliko ukoloni mamboleo?
Prof.: Utandawazi ni remote control yenu una ukweli, lakini pale tu watu wanapokuwa wajinga. Werevu una nguvu zaidi kuliko remote control (uk. 61).
Prof. ana imani kuwa wao watashinda katika makabiliano haya mapya. Anamweleza Sheta kuwa anashangaa ni kwa namna gani wao Waafrika walidanganyika hapo awali wakadhani Mzungu alikuwa na uwezo mkubwa waliouona kama miujiza. Kwamba wameamka na kile walichodhani ni ustaarabu wa hali ya juu (utandawazi) wakautambua kuwa mazingaombwe tu (uk. 72). Nao wananchi wanamhakikishia Prof. kuwa hawatachoka. Wataendelea na juhudi zao hadi mwisho pale ambapo watamshinda adui kikamilifu (uk. 76).
Wananchi wanajitolea kwa kila hali kutaka haki yao kutoka kwa wakoloni Wazungu na kwa viongozi wao wakoloni. Wanaamua kuandamana njiani huku wakitoa kauli mbalimbali kushinikiza watakacho. Wanasema:
Umma: Sisi ni wananchi… Hii ni nchi yetu… Hatutaki kutawaliwa kwa remote control… rasilimali zetu ziwe mikononi mwa wenyeji… Biashara iwe nipe nikupe. Viongozi wetu wawe macho… Viongozi wetu wawe na sisi wasiwena mashetani… (uk. 74).
Kwa kudai kuwa viongozi wao wawe nao, wasiwe na mashetani wanaashiria kuwa wanajua na kutambua kuwa viongozi wao walikuwa wanashirikiana na wakoloni Wazungu kuwanyanyasa wananchi. Hivi ni kusema kuwa kulikuwapo na viwango hivyo viwili vya ukoloni, jambo ambalo lilidhihirisha mzigo mkubwa kwa mwananchi.
Huku Wazungu wakija Afrika kuwapora raslimali zao, Waafrika wenyewe hawaendi kupora raslimali za Wazungu. Badala yake, wakienda huko wanaenda kunyanyaswa nguvu zao zaidi kwa manufaa ya wenyeji wa huko. Matokeo ya jambo hili ni Waafrika kuendelea kuwa maskini jinsi ambavyo Wazungu wanaendelea kutajirika. Lakini wale Waafrika waliozinduka na kung’amua hali hii wanaamua kubakia nchini mwao. Tunasoma hivi:
Prof.: … sijapanga kwenda pahali pengine. Nitaselelea papa hapa petu.
Sheta: Ndiyo maana utabakia maskini (uk. 78).
Maneno ya Sheta yananuia kumshawishi Prof. aamini kuwa kule Uzunguni ndiko kwenye utukufu na utajiri. Kwamba kilichoko Afrika ni maovu na umaskini.
Mtu mweusi kama msingi wa ustaarabu
Nadharia ya ujumi mweusi inaadhimisha wazo kwamba mtu mweusi ndiye msingi wa ustaarabu kote ulimwenguni. Hii ina maana kuwa maendeleo na uimarikaji wa Uzunguni kiuchumi ni zao la matumizi ya nguvu za Waafrika. Prof. anamkumbusha Sheta ukweli huu alipokuwa akimjibu madai yake kwamba Wazungu wamekuza uchumi wao kwa juhudi zao tu.
Sheta: Hatuutegemei tena mbuyu.Uwe wa jana au wa leo. Tunachokitegemea ni nguvu na akili zetu tu.
Prof.: (Kinamtoka kicheko kikubwa cha kejeli na tashtiti.) Bila ya nguvu zetu, zenu hazifui dafu. (uk. 24).
Suala hili linasisitizwa na Mzee Jumai alipokuwa akimjibu Sheta. Anamwambia kuwa Wazungu hawaishi kukusanya na kuiba nguvu za Waafrika. Anaongeza huwa hata wakati mwingine wanafikia malengo haya ya kuiba nguvu hizo kwa kutumia sheria fulani walizoziweka wao (uk. 44). Kung’amua huku kunapaswa kufuatwa na Waafrika kujifunga katoka kutumia nguvu kuimarisha uchumi wa mataifa yao badala ya yale ya nje. Kijana 1 vilevile anamkumbusha Sheta kwamba ukuaji wa kiuchumi wanaojivunia na juhudi za Waafrika. Aghalabu Waafrika walifanya hivyo bila hiari yao. Hii ndio maana Kijana 1 anasema hivi: ‘Aaa, miaka mingi mmezibana akili zetu ili mweze kufyonza damu yetu’ (uk. 48).
Hitimisho
Makala haya yameweza kuonyesha kuwa tamthilia ya Kiswahili imeweza kuimarika sana katika kufumbata hali halisi ya Mwafrika. Imejidhihirisha kama chombo cha Mwafrika cha kujinasua kutokana na athari za muda mrefu alizopata tangu wakati wa utumwa hadi leo wakati wa utandawazi. Makala yameweka bayana kwamba Mwafrika ameweza kuzinduka vilivyo na kuona makosa yake. Haya ni makosa ambayo amekuwa akifanya, na kwa kufanya hivyo akamrahisishia mkoloni amnyanyase kwa kipindi chote hicho. Amejifaragua na kusimama kidete kutetea utu, heshima, rangi na kila kilicho na asili ya Kiafrika. Kwamba kuwa Mwafrika, na mtu mweusi kwa rangi sio ulemavu. Ni ustaarabu na nguvu. Ustaarabu ulioenea kote ulimwenguni, na nguvu ambazo ndizo chemchemi za ustaarabu katika mataifa yanayojiita makubwa kote ulimwenguni.
Marejeleo
Curtin, P. D (1964). The Image of Africa: British Action 1780-1850. Wisconsin: University of Wisconsin Press.
Cesaire, A. (1968). Return to My Native Land. Paris: Presence Africaine.
Mohamed, S.A (2016). Mashetani Wamerudi. Nairobi: Spotlight Publishers.
Molefi, K. A (1999). The Painful Demise of Eurocentricism. Trenton: African World Press.
Wafula, R.M na Njogu K. (2007). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: JKF.
Zirimu, Pio na wengine, ed. (1971). Black Aesthetics. Nairobi: EALB.
Tathmini Ya Ujumi Mweusi Katika Tamthilia Ya Mashetani Wamerudi (S.A.M 2016)