Mifanyiko Ya Unyambulishaji Wa Vitenzi Katika Kigĩchũgũ
1Magdalene Wangu Gituru & 2John M. Kobia
1,2 Chuo Kikuu cha Chuka
Ikisiri
Unyambulishaji wa vitenzi ni mojawapo ya masuala yanayoshughulikiwa katika taaluma ya mofolojia katika lugha nyingi za Kiafrika. Makala hii inashughulikia unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ, mojawapo ya lugha za kiafrika, kwa kufafanua mifanyiko inayohusika katika utaratibu wa unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ na kutathmini kanuni zinazoruhusu au kuzuia mifanyiko hiyo ya unyambulishaji. Katika uainishaji wa Guthrie (1967), Kigĩchũgũ ni mojawapo ya lugha za Kiafrika ambayo hudhihirisha unyambulishaji. Nadharia ya Mofolojia Leksia (Kiparsky 1982 na Katamba 1993) na Kanuni ya Kioo (Baker 1985) zimetumiwa kueleza mfuatano wa mofimu nyambulishi katika vitenzi vya Kigĩchũgũ. Data ya vitenzi sitini (60) vya Kigĩchũgũ ilitumika katika makala hii. Vitenzi hivi viliwekwa katika kauli sita za unyambulishaji na kuainisha mifanyiko inayohusika katika utaratibu wa unyambulishaji kwa kutumia jedwali la mnyambuliko wa vitenzi. Makala hii inachangia katika kuongeza maarifa ya kiutafiti kuhusu sarufi ya Kigĩchũgũ na kuhifadhi lugha ya Kigĩchũgũ kama mojawapo ya lugha za Kiafrika katika maandishi.
Maneno makuu; Unyambulishaji, Mifanyiko, Vitenzi, Kigĩchũgũ
Utangulizi
Unyambulishaji ni aina mojawapo ya uambikaji. Kwa mujibu wa Gawasike (2012), uambikaji ni upachikaji wa mofu kabla na baada ya mzizi wa neno na ambao umegawika katika sehemu mbili; uambishaji na unyambulishaji. Anaeleza kuwa mgawanyo wake ni mzizi wa neno. Uambikaji ni dhana ya juu (kiambajengo cha juu) ikiundwa na viambajengo sisisi ambavyo ni uambishaji na unyambulishaji. Unyambulishaji ni mojawapo ya mifanyiko inayotokea katika kitenzi. Waihiga (1999: 152), anafafanua kuwa unyambulishaji hutokana na vitenzi viwili ambavyo ni nyambua na nyumbua. Anaeleza kunyambua kama kukata kitu vipande vipande na kunyumbua kama kuvuta vitenzi ili kuvirefusha hivyo kuunda kauli mbalimbali za unyambulishaji. Kwa mujibu wa Kihore, Massamba na Msanjila (2012), unyambulishaji ni upachikaji wa viambishi kwenye mzizi ili kuunda maneno mapya. Wanaendelea kusema kuwa katika lugha ya Kiswahili kuna viambishi nyambulishi ambavyo hutumika katika uundaji wa vitenzi vipya. Kihore, Massamba na Msanjila (wataje) wanafafanua unyambulishaji wa vitenzi kama utaratibu wa uundaji wa vitenzi vipya katika lugha kwa kuongeza viambishi nyambulishi kwenye maumbo ya mzizi. Kwa mfano kitenzi #piga# kinanyambuliwa kwa kufuata utaratibu huu ambao hufanyika katika hatua kama vile:
piga
Pig-w-a
Pig-an-a
Pig-i-a
Pig-i-an-a
Pig-i-w-a
Pig-an-ish-a
(Asili: Kihore, Massamba na Msanjila, 2012: 122)
Kihore, Massamba na Msanjila (2012) wanaeleza kuwa hatua ya kwanza ni ile ya kiambishi kinachofuata mzizi moja kwa moja kama inavyodhihirika katika mifano a), b) na c); na hatua ya pili ni ya kiambishi nyambulishi cha pili kutoka kwenye mzizi kama inavyodhihirika katika mifano d), e) na f
Heine na Mohlig (1980: 20) wanatilia mkazo kuwa lugha nyingi nchini Kenya zina utaratibu fulani wa unyambulishaji wa vitenzi. Wanasema kuwa nchini Kenya lugha zinaweza kugawika katika makundi mawili: Kundi la kwanza ni la lugha zilizopungukiwa katika mofolojia ya uundaji wa maneno ambazo wataalamu hawa wanasema kuwa huwa na kauli chache za unyambulishaji wa vitenzi. Kundi la pili ni la lugha zilizoimarika katika mofolojia ya uundaji wa maneno na ambazo huwa na kauli nyingi za unyambulishaji wa vitenzi. Baadhi ya kanuni za unyambulishaji wanazozitambua ni pamoja na kauli ya kutendwa, kutendesha, kutendea, kutendua, kutendana miongoni mwa zingine.
Kigĩchũgũ ni mojawapo ya lugha za Kikuyu inayozungumzwa katika Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya. Kaunti hii hupakana na Kaunti ya Nyeri upande wa Kaskazini Magharibi, Kaunti ya Murang’a upande wa Magharibi na Kaunti ya Embu upande wa Mashariki na Kusini. Kaunti ya Kirinyaga imegawanywa katika Kaunti ndogo tano; Kirinyaga ya Mashariki, Kirinyaga Magharibi, Kirinyaga ya Kati, Mwea Mashariki na Mwea Magharibi. Kigĩchũgũ huzungumzwa na wakaazi ambao hupatikana katika Kaunti ndogo ya Kirinyaga Mashariki.
Kwa mujibu wa Mutahi (1977) Kigĩchũgũ ni miongoni mwa lahaja za mashariki. Lahaja zingine ni kama vile, Kiembu, Kimbeere, na Kindia. Mutahi (keshatajwa), anasema kuwa wazungumzaji wa lahaja ya Kigĩchũgũ huwa kati ya mto Rupingazi na Thiba. Anasema kuwa Rupingazi huwatenga na Wagichũgũ na Waembu nao Thiba huwatenga na Kindia. Anaendelea kusema kuwa mpaka halisi kati ya Ndia na Gĩchũgũ ni mto Rutui. Kulingana na sensa za mwaka wa 2009, tarafa ya Gĩchũgũ ambayo ndiyo kitovu cha wazungumzaji halisi wa Kigĩchũgũ ilikuwa na wazungumzaji elfu mia moja ishirini na nne, mia sita sabini na mbili (124,672). Kulingana na Mipango ya Maendeleo ya Kaunti ya Kirinyaga mwaka wa 2018-2022, wazungumzaji wa Kigĩchũgũ mwaka wa 2019 wanakisiwa kuwa elfu mia moja arobaini na nne, mia nane arobaini na nane (144,848). Uainishaji wa Guthrie (1967) ulipangilia lugha ya Kikuyu katika kundi la E51. Kwa mujibu wa Nurse na Philippson (2003), lugha ya Kibantu ni kundi la lugha ambalo ni tawi la lugha za Niger-Kongo. Wanatambua kwamba jamii za Kibantu huishi Afrika. Katika maelezo yao, wanatambua Kikuyu miongoni mwa lugha za Kibantu. Wanaendelea kusema kuwa lugha za Kibantu zimeimarika sana katika mofolojia ya uundaji wa maneno na mofolojia ya unyambulishaji wa vitenzi.
Schadeberg (2003) anaeleza kuwa vitenzi vya Kibantu vina uwezo mkubwa wa mzizi kubeba viambishi aidha vya nafsi, njeo, urejeshi na hata viambishi vya unyambulishaji. Kutokana na maelezo yake Schadeberg (mtaje), kitenzi cha Kigĩchũgũ kina uwezo mkubwa wa kubeba viambishi kuliko aina zingine za maneno katika lugha hii. Kama ilivyo katika Kiswahili, vitenzi vya Kigĩchũgũ huchukua viambishi awali na viambishi tamati hivyo basi makala hii inashughulikia viambishi tamati kwani ndivyo hupachikwa baada ya mzizi wa vitenzi katika mfanyiko wa unyambulishaji.
Lengo la Makala
Makala hii iliongozwa na lengo la kufafanua mifanyiko inayohusika katika utaratibu wa unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ.
Unyambulishaji wa Vitenzi katika Lugha za Kiafrika
Suala la unyambulishaji wa vitenzi limeshughulikiwa na wataalamu kama vile; Kiango (2008) anasema kwamba, michakato yote ya unyambulishaji katika Kiswahili inatawaliwa na kanuni za kifonolojia na kimofolojia. Anaendelea kusema kuwa kanuni za unyambulishaji vitenzi ambazo zinatumiwa katika mizizi au mashina ya vitenzi zinazalisha aina mbalimbali za unyambuaji tenzi. Baadhi ya aina hizo ni kama vile; unyambuzi- tendea, unyambuzi- tendana, unyambuzi- hali, unyambuzi-tendeshana unyambuzi-tendwa.
Unyambulishaji wa vitenzi ya Kigryama umeshughulikiwa na Ngowa (2008) huku akionyesha jinsi Kigryama ni lugha ya Kibantu kwa kurejelea dhana ya kitenzi. Katika utafiti wake, anatumia mtazamo wa fonolojia leksishi ambao unatambua kuwa uambishaji wa maneno unaandamana na mageuzi au sheria za kifonolojia za kiwango kimoja. Katika utafiti wake anashughulikia muundo wa ndani wa kitenzi akiegemea pia katika eneo la mofolojia. Anatambua kwamba kitenzi cha Kigryama kina uwezo mkubwa wa kubeba viambishi kuliko aina zingine za maneno. Amezingatia kikamilifu jinsi kanuni za fonolojia leksishi zimetumiwa ili kuongoza unyambulishaji wa vitenzi.
Akishughulikia unyambulishaji wa vitenzi katika lugha ya Runyankole, Asiimwe (2011), alijadili mofimu za Utendea, Usababishi, Utendeka na Utendwa. Alibainisha kuwa unyambulishaji wa vitenzi katika Runyankole, mojawapo ya lugha za Kiafrika, unahusisha mizizi ya vitenzi ambapo mofimu nyambulishi hupachikwa. Anatambua kwamba mofimu nyambulishi za usababishi hupokezwa kitenzi kwanza kabla ya utendwa. Anaeleza kuwa usababishi huunda kitenzi elekezi kutokana kile ambacho sielekezi kwa sababu vitenzi elekezi tu ndivyo vinaweza kupokea utendwa.
Charwi (2013), alishughulikia unyambulishaji wa vitenzi katika Kikuria akiwa na lengo la kueleza matokeo ya vitenzi vya Kikuria baada ya unyambulishaji na idadi ya viambishi vinavyoweza kuwekwa pamoja kwenye kitenzi. Alichanganua unyambulishaji wa vitenzi ili kuonyesha dhana ya uelekezi unavyojitokeza na kuonyesha upekee na ufanano wa lugha ya Kikuria na lugha nyingine za Kibantu kama vile, Kinyambo, Kinyamwezi, Kibosho miongoni mwa lugha zingine. Utafiti wa Charwi (mtaje) ulilenga kufafanua athari za unyambulishaji kisintaksia. Aidha, anagundua kuwa vitenzi vya Kikuria kama ilivyo kwenye lugha nyingi za Kibantu huwa na sifa tofauti tofauti kulingana na aina ya kitenzi. Kwa mfano, anasema kuwa vitenzi si elekezi havihitaji yambwa wakati vitenzi elekezi huhitaji yambwa moja au mbili kulingana na asili ya kitenzi chenyewe. Katika kazi yake anatambua kauli ya utendea, usababishi, utendano, utendwa na utendeka. Anaeleza kuwa athari ya vitenzi hivi hutofautiana kutokana na aina za viambishi vilivyopachikwa kwenye mizizi ya vitenzi hivyo.
Akishughulikia Mofosintaksia katika vitenzi vya Keiyo, Jepkoech (2018) alitambua na kujadili mofimu ambishi na nyambulishi. Alilenga kutambua ruwaza za upachikaji katika mpangilio wa vitenzi na kuchanganua kanuni za kimofosintaksia zinazoathiri upachikaji wa viambishi katika kitenzi cha Keiyo. Mtafiti aliongozwa na Nadharia ya Kioo. Katika kazi yake, Jepkoech (keshatajwa) alitambua kwamba mofimu ambishi hutokea mwanzoni mwa kitenzi cha Keiyo isipokuwa zile ambazo huonyesha wakati uliopo na hali ya kuendelea. Alitambua pia kuwa mofimu nyambulishi hutokea mwishoni baada ya mzizi. Katika kazi yake, mtafiti alionyesha kuwa mofimu ambishi hufuata utaratibu wa wakati → ukanusho → hali → nafsi → mzizi. Kwa upande mwingine, alionyesha kuwa mofimu nyambulishi huchukua taratibu mbalimbali.
Misingi ya Kinadharia
Utafiti huu ulijikita katika misingi ya nadharia ya Mofolojia Leksia (ML). Kwa mujibu wa Kiparsky (1982) na Katamba (1993) nadharia ya Mofolojia Leksia iliibuka kufidia mtazamo wa Chomsky wa sarufi zalishi (SZ) ambao haukutambua kiwango cha mofolojia kama kiwango mahususi cha lugha. Katamba (mtaje) amefafanua Nadharia ya Mofolojia Leksia kwa kuzingatia uambishi wa maneno kwa jumla ikiwemo vitenzi. Nadharia ya Mofolojia Leksia (ML) inatambua viwango viwili vya sheria: sheria leksia na sheria kirai. Sheria Leksia ni zile ambazo zinafungamana na kanuni za kifonolojia katika kuunda neno husika kwa namna ambavyo umbo la mzizi hubadilika linapoongezewa viambishi katika neno. Sheria Kirai huathiri kiambishi katika neno kwa kukipitisha mageuzi yanayohusu vokali zinazopatikana.
ML inahusisha mihimili sita ya uamilifu wa sheria mahususi za kisarufi. (Katamba 1993). Mihimili hii ni; ngazi leksia, mzunguko wa sheria, kufuta mabano, kwingineko, kuhifadhi muundo na ufinyu wa sifa. Mihimili minne ndiyo iliyotumika katika uchanganuzi wa unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ.
Kwanza, mhimili wa ngazi leksia unazingatia kwamba umbo la neno linaweza kuelezwa kupitia maumbo ya kisarufi yaani mofimu zenye daraja za mahusiano. (Kiparsky, 1982 na Katamba (1993). Kwa mfano, kitenzi cha Kigĩchũgũ [kuruga] (kupika) kina maumbo kama yafuatayo:
Ngazi leksia katika kitenzi [kuruga]
Maumbo haya yametenganishwa kwa kuzingatia ngazi ambapo kila umbo lina maana bainifu ya kisarufi. Ngazi hizi huwa zenye mahusiano na zinapotenganishwa haziwezi kutoa maana yoyote. Kwa mfano /rug/ peke yake haina maana yoyote mpaka iunganishwe na kiambishi awali /kũ/ pamoja na kiishio /a/ ili kutoa maana ya #kũruga# (kupika). Aidha kiishio /a/ na kiambishi awali /kũ/ havina maana yoyote hadi pale ambapo vinapounganishwa na mzizi /rug/ wa kitenzi husika. Umuhimu wa kanuni hii katika makala ni kuwa unyambulishaji hufanywa kwa utaratibu ambao hufanyika kwa hatua.
Pili, mhimili wa kufuta mabano unazingatia kwamba wakati sheria ya kiwango kimoja ya kifonolojia imetumika, mabano yake hufutwa mpaka mwishowe neno lenye umbo kamili na maana ya kileksia pamoja na umbo la kimofolojia hupatikana. Mhimili huu umetumika kwa sababu umeonyesha kwamba hata baada ya mageuzi ya unyambulishaji wa vitenzi, maumbo mbalimbali huungana na kuwa kitenzi kimoja kamili.
Tatu, mhimili wa kuhifadhi muundo hutambua kwamba baada ya mageuzi ya kifonolojia, muundo wa lugha mahususi sharti uhifadhiwe (Katamba 1993). Kwa mfano, muundo wa lugha za Kibantu ukiwemo Kigĩchũgũ ni ule wa mfuatano wa Konsonanti-Vokali (K-V). Kitenzi cha Kigĩchũgũ /kũ+iya/ [kwiya] (kuiba) kimeweza kutoa kielelezo bora. Uchopekaji wa kiishio {a} unafunga mzizi wa kitenzi kwa vokali. Uyeyushaji wa vokali /u/ katika kiambishi awali unazalisha fonimu changamano {kw} ambayo inatamkwa kama fonimu moja hivyo basi umbo bora la K-V linadumishwa.
Nne, mhimili wa kwingineko hutumiwa pale ambapo sheria mbili huonekana kushindania nafasi moja. Hali hii hudhihirika katika mofolojia ambapo baada ya uambishi awali katika vitenzi vokali mbili huwa zinafuatana. Jambo hili litokeapo, udondoshaji wa vokali na uyeyushaji wa vokali hutumikizwa (Katamba, 1993). Hata hivyo, mhimili wa kwingineko unapendekeza uyeyushaji wa vokali kwa sababu udondoshaji hutumika katika mazingira mengi. Mfano wa kitenzi [kwina] (kuimba) unadhihirisha uyeyushaji wa vokali. Hii ni kwa sababu kitenzi hiki kina vokali mbili ambazo zinafuatana yaani: [kuina]. Vokali /u/ inapitia uyeyushaji na kuwa /w/ badala ya kudondoshwa.
Nadharia ya ML ilifaa katika makala hii kwani ilisaidia kuonyesha jinsi kanuni za kifonolojia na kimofolojia hushirikiana katika unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ. Kanuni ya kioo ilitumika katika makala hii kwani kulingana na Baker (1985) kanuni hii ni kanuni sarufi inayopendekeza kuwa unyambulishaji ni lazima uakisi mfuatano wa kisintaksia na kinyume chake. Kwa mujibu wa Baker (mtaje) unyambulishaji wa vitenzi katika lugha za Kibantu hufuata mpangilio maalum wa unyambulishaji wa vitenzi. Kanuni hii inafaa makala hii kwani ilisaidia katika kushughulikia mifanyiko inayohusika na unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ mojawapo ya lugha za Kibantu.
Ukusanyaji wa Data
Ili kupata data ya unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ, watafiti walishiriki katika kutunga sentensi ambapo walichagua vitenzi sitini (60) katika lugha ya Kigĩchũgũ ambavyo walivipanga katika jedwali la usaili wa vitenzi vya Kigĩchũgũ kwa kushughulikia kauli sita za unyambulishaji na kuainisha kanuni za mageuzi katika Kigĩchũgũ. Idadi hii ilichaguliwa kutumika katika makala hii kwa sababu kulingana na Milroy (1987), tafiti za kiisimu, kama ilivyo makala hii, zinajulikana kuzalisha data yenye uradidi mwingi. Maoni yake ni kuwa kadri data ilivyo kubwa ndivyo kuna uwezekano wa uradidi. Aidha, kwa mujibu wa Chomsky (1957) mzawa wa lugha ana uwezo wa kuzalisha sentensi nyingi sahihi na zisizo na kikomo hivyo basi watafiti kama wazawa na wazungumzaji wa Kigĩchũgũ waliweza kuzalisha vitenzi ambavyo vilitumika katika makala hii na kuvithibitisha kupitia kwa data ambayo walipata kutoka kwa wazungumzaji wengine wa Kigĩchũgũ .
Uchanganuzi wa Data
Kwa mujibu wa Wesana- Chomi (2013), unyambulishaji ni mchakato au mfanyiko wa kuambatisha kiambishi kimoja au zaidi kwenye mzizi wa vitenzi ili kuunda vitenzi vingine. Vitenzi vya Kigĩchũgũ vina uwezo wa kuambishwa viambishi kwenye mzizi ili kudhihirisha maana tofauti. Vitenzi vya Kigĩchũgũ hurusu uambishaji tamati katika vitenzi husika. Viambishi tamati ni mofimu ambazo hupachikwa baada ya mzizi wa vitenzi katika mfanyiko wa unyambulishaji. Makala hii imeshughulikia unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ kwa kujadili kauli sita za unyambulishaji: kutendea, kutendwa, kutendesha, kutendana, kutendeka na kutendua kwa kutilia maanani mifanyiko inayohusika katika unyambulishaji wa vitenzi. Katika kazi hii, nadharia ya mofolojia leksia (Kiparsky 1982 na Katamba 1993) na Kanuni ya Kioo (Baker 1985) zimetumiwa ili kueleza mfuatano wa vinyambulishi katika lugha ya Kigĩchũgũ na kutathmini kanuni zinazoruhusu na kuzuia mifanyiko hiyo ya unyambulishaji. Vitenzi hivi vimewekwa katika kauli sita ili kudhihirisha kanuni na sheria zinazotawala mifanyiko ya unyambulishaji katika Kigĩchũgũ. Kauli hizi ni pamoja na:
Kauli ya Kutendea (TDA)
Kauli ya kutendea katika Kigĩchũgũ huweza kuwa na viambishi nyambulishi viwili kutegemea irabu zilizo kwenye mzizi wa kitenzi. Viambishi hivi ni kama vifuatavyo:
Kinyambulishi { –ĩr-}
Katika Kigĩchũgũ, kauli ya TDA huchukua mofimu {-ĩr-} kabla ya irabu ya mwisho kwenye vitenzi katika unyambulishaji. Mofimu hii hutumika iwapo mzizi wa kitenzi una irabu /a/, /i/, / ĩ /, /ũ/au /u/. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
maana |
Kauli ya Kutendea |
1 |
thak-a |
cheza |
thak-ĩr-a |
2 |
bing-a |
funga |
bing-ĩr-a |
3 |
rĩm-a |
lima |
lim-ĩr-a |
4 |
rũg-a |
ruka |
rug-ĩr-a |
5 |
bur-a |
panguza |
bur-ĩr-a |
Kinyambulishi {-er-}
Katika Kigĩchũgũ, kinyambulishi {-er-} huchopekwa kwenye unyambulishaji wa vitenzi iwapo mzizi wa vitenzi una irabu /e/ na /o/. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
maana |
Kauli ya Kutendea |
6 |
thom-a |
soma |
thom-er-a |
7 |
tem-a |
kata |
tem-er-a |
8 |
boy-a |
omba |
bo-er-a |
Kupitia maelezo haya katika kauli ya TDA, viambishi {-ĩ-} na {-e-} vimetumika katika unyambulishaji. Hata hivyo kiambishi {-r-} kimetumika pia ili kuhifadhi muundo wa Kigĩchũgũ wa Konsonanti-Vokali (K-V) kama inavyopendekezwa na Katamba (1993) kwamba baada ya mageuzi ya kifonolojia, muundo wa lugha mahususi sharti uhifadhiwe. Kwa upande mwingine, kama anavyosema waithaka (2010), irabu ya mzizi katika kauli ya TDA hukubaliana na kiambishi nyambulishi kinachofuata. Hali hii ya ukubalifu anairejelea kama uwiano wa vokali. Kutokana na maelezo ya kauli ya TDA katika Kigĩchũgũ, inabainika kuwa iwapo mzizi wa kitenzi una irabu ya juu yaani /i/ na /u/, basi kinyambulishi cha kati-juu yaani /ĩ/ kilitumika. Vilevile, mzizi wenye irabu ya chini /a/, kinyambulishi cha kati-chini /e/ kilitumika.
Kauli ya Kutendwa (TDW)
Vitenzi katika Kigĩchũgũ, hupachikwa kiambishi {-w-} katika unyambulishaji ili kudhihirisha kauli ya utendwa. Kiambishi hiki hupachikwa baada ya mzizi wa vitenzi vinavyoishia kwa konsonanti. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
maana |
Kauli ya Kutendwa |
9 |
men-a |
chukia |
men-w-a |
10 |
nyit-a |
shika |
nyit-w-a |
11 |
cor-a |
chora |
cor-w-a |
12 |
mund-a |
dunga |
mund-w-a |
Mifano iliyoonyeshwa hapo juu inadhiihirisha kwamba irabu /u/ inayeyushwa na kuwa /w/ baada ya unyambulishaji. Kwa mfano,
men-u-a (men-w-a)
nyit-u-a (nyit-w-a)
mund-u-a (mund-w-a).
Hii ni kulingana na mhimili wa kwingineko katika nadharia ya ML, ambao unapendekeza kuwa, iwapo katika mofolojia irabu mbili zinafuatana na kushindania nafasi, uyeyushaji utumikizwe (Katamba 1993).
Kwa upande mwingine, baadhi ya vitenzi vya Kigĩchũgũ vinavyoishia kwa irabu /i/, hupachikwa kinyambulishi {-u-} katika kauli ya kutendwa. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendwa |
13 |
Giri-a |
zuia |
Gir-u-a |
14 |
Tini-a |
kata |
Tin-u-a |
15 |
Tongori-a |
ongoza |
Tongor-u-a |
16 |
Kethi-a |
salimu |
Keth-u-a |
Katika mifano hii ya vitenzi vya Kigĩchũgũ, irabu /i/ inadondoshwa na /u/ kuachwa kama kiambishi cha kauli ya kutendwa. Irabu /i/ inadondoshwa kwa sababu Kigĩchũgũ hakikubali mfuatano wa irabu tatu. Baada ya udondoshaji, irabu /u/ huyeyushwa na kuwa /w/. Hii ni kwa msingi wa Nadharia ya ML
Kauli ya Kutendesha (TSH)
Kauli ya kutendesha katika Kigĩchũgũ huonyeshwa kwa kiambishi {-ithi-} katika unyambulishaji wa vitenzi. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendesha |
17 |
ak-a |
jenga |
ak-ithi-a |
18 |
end-a |
penda |
end-ithi-a |
19 |
tum-a |
shona |
tum-ithi-a |
20 |
ken-a |
furahi |
ken-ithi-a |
21 |
rĩb-a |
lipa |
rĩb-ithi-a |
Vilevile, kauli ya kutendesha katika Kigĩchũgũ huonyeshwa kwa kiambishi {-i-} katika baadhi ya vitenzi ambavyo kisemantiki huonyesha anayesababisha kitendo kama mshiriki. Vitenzi hivi kwa kawaida ni vitenzi si elekezi. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendesha |
22 |
rwar-a |
ugua |
rwar-i-a |
23 |
in-a |
imba |
in-i-a |
24 |
tet-a |
teta |
tet-i-a |
25 |
nor-a |
nenepa |
nor-i-a |
26 |
gamb-a |
toa sauti |
gamb-i-a |
Kutokana na mifano iliyotolewa katika kauli ya TSH, kiambishi nyambulishi {-ithi-} hutumika katika vitenzi elekezi ilhali kiambishi nyambulishi {-i-} hutumika katika vitenzi vya Kigĩchũgũ ambavyo si elekezi. Hata hivyo wakati mwingine, kiambishi {-ithi-} huweza kutumika na vitenzi si elekezi pia. Kiambishi {-ithi-} cha kauli ya TSH kinaonekana kuwa kizalishi kwa kiasi kikubwa kuliko kiambishi {-i-} ambacho kinatumika kwa vitenzi vichache.
Kauli ya Kutendana (TDN)
Kauli ya kutendana katika Kigĩchũgũ huonyesha kuwa wahusika wawili au zaidi kufanyiana kitendo kimoja. Kauli ya kutendana katika unyambulishaji wa baadhi ya vitenzi katika Kigĩchũgũ huonyeshwa kwa kiambishi {-an-} kama inavyodhihirika katika mifano ifuatayo.
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendana |
27 |
bũr-a |
chapa |
bũr-an-a |
28 |
kuu-a |
beba |
ku-an-a |
29 |
rũg-a |
ruka |
rũg-an-a |
30 |
thik-a |
zika |
thik-an-a |
7 |
tem-a |
kata |
tem-an-a |
Kauli ya Kutendeka (TDK)
Kama ilivyoelezwa katika kauli ya kutendea, kauli ya kutendeka pia huweza kuwa na viambishi nyambulishi viwili kama ifuatavyo;
Kinyambulishi {-ek-}
Kinyambulishi {-ek-} katika unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ huchopekwa kabla ya kiambishi tamati iwapo mzizi wa vitenzi hivyo una irabu /o/ na /e/. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendeka |
31 |
kom-a |
lala |
kom-ek-a |
32 |
oc-a |
chukua |
oc-ek-a |
9 |
men-a |
chukia |
men-ek-a |
33 |
meny-a |
fahamu |
meny-ek-a |
Kinyambulishi {–ĩk-}
Vitenzi katika Kigĩchũgũ huchopekwa kiambishi {-ĩk-} kabla ya kiambishi tamati katika unyambulishaji iwapo mzizi wa vitenzi hivyo una irabu /a/, /i/, /ĩ/, /ũ/ na /u/. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendeka |
||
34 |
tham-a |
hama |
tham-ĩk-a |
||
10 |
nyit-a |
shika |
nyit-ĩk-a |
||
35 |
rĩr-a |
lia |
rĩr-ĩk-a |
||
36 |
kũnj-a |
kunja |
kũnj-ĩk-a |
||
37 |
ug-a |
sema |
ug-ĩk-a |
||
Kama ilivyo katika kauli ya kutendea, kiambishi {-e-} na [-ĩ-} vimetumika katika unyambulishaji. Hata hivyo, kiambishi {-k-} pia kimetumiwa ili kuhifadhi muundo wa Kigĩchũgũ wa Konsonanti-Vokali.
Kauli ya Kutendua (TDU)
Vitenzi katika kauli ya kutendua katika Kigĩchũgũ hutoa maana iliyo kinyume cha kitenzi katika kauli ya kutenda. Viambishi vya unyambulishaji katika kauli ya kutendua katika Kigĩchũgũ ni {-ũr-} na {-or-}. Mofimu {-ũr-} hupachikwa kwenye vitenzi vyenye mzizi wenye irabu /a/, /i/, /u/ na /ũ/ ilhali {-or-} hupachikwa kwenye vitenzi vyenye mzizi wenye irabu /o/. Kwa mfano,
|
Kitenzi |
Maana |
Kauli ya Kutendua |
38 |
bing-a |
funga |
bing-ũr-a |
39 |
ak-a |
jenga |
ak-ũr-a |
19 |
tum-a |
shona |
tum-ũr-a |
30 |
thik-a |
zika |
thik-ũr-i-a |
36 |
kũnj-a |
kunja |
kũnj-ũr-a |
40 |
ob-a |
funga (kwa mfano kamba) |
ob-or-a |
41 |
rog-a |
roga |
rog-or-a |
Ingawa vitenzi vya Kigĩchũgũ katika kauli ya kutendua huonyesha kinyume, ni muhimu pia kutambua kuwa vitenzi hivi vinaweza kunyambulishwa zaidi katika kauli zingine. Kwa mfano,
tendua |
tendea |
tendwa |
tendesha |
tendeka |
kũnjũra |
kũnjũrĩra |
kũnjũrwa |
kũnjũrithia |
kũnjũka |
obora |
oborera |
oborwa |
oborithia |
oboka |
Mfuatano wa Viambishi Nyambulishi katika Kigĩchũgũ
Unyambulishaji katika vitenzi vya Kigĩchũgũ huweza kuchukua mwambatano wa viambishi vingi vya unyambulishaji kwa wakati mmoja. Kama wanavyosema Kihore, Massamba na Msanjila (2012:127), viambishi nyambulishi huandamana na mizizi hatua kwa hatua. Hii ina maana kuwa kiambishi huandama kiambishi nyambulishi na kingine au vingine kufanya vivyo hivyo. Wanasema kuwa vitenzi vya Kiswahili vinaweza kufikia hadi hatua nne za unyambulishaji.
Kwa mujibu wa Wesana-Chomi (2013), kitenzi kimoja kinaweza kuchukua vinyambulishi viwili au zaidi. Hata hivyo, anaeleza kuwa vinyambulishi hivi havitokei ovyo bali huongozwa na kanuni mbalimbali ambazo zinahusika katika unyambulishaji huo.
Hyman (2003) anasema kuwa mizizi ya vitenzi katika lugha za Kibantu huweza kuchukua viambishi nyambulishi mbalimbali ili kuwakilisha maana tofauti. Hyman (keshatajwa), anapendekeza mfuatano wa CARP yaani C- causative (usababishi), A- Applicative (utendea), R- Reciprocal (utendano) na P- Passive (utendwa) ambao hutambua hatua nne za unyambulishaji katika lugha za Kibantu. Makala hii ilifafanua mifuatano ya mofimu nyambulishi katika Kigĩchũgũ ili kubaini iwapo inaaafiki au kukiuka ule mfuatano uliopendekezwa na Hyman (mtaje).
Kigĩchũgũ kama lugha zingine za Kibantu hufuata mwambatano wa viambishi vinyambulishi viwili au zaidi. Mifano iliyojadiliwa katika kauli sita za unyambulishaji, inahusu hatua ya kwanza ya viambishi nyambulishi vya Kigĩchũgũ vinavyofuata mizizi moja kwa moja. Mifano inayofuata imezingatia unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ katika hatua ya pili, ya tatu na ya nne.
Mfuatano wa Viambishi Nyambulishi Viwili
Kama anavyopendekeza Waweru (2011) kuhusu mifuatano nyambulishi katika Gĩkũyũ, Kigĩchũgũ pia kinaweza kuwa na viambishi nyambulishi viwili. Mifuatano hii ni pamoja na;
Kauli ya Kutendea na Kutendwa (TDA+TDW)
Mofimu zinazowakilisha kauli ya kutendea katika Kigĩchũgũ ni {-ĩr-} na {-er-} na kauli ya kutendwa ni {-w-}. Mifano ifuatayo inaonyesha kuwa Kigĩchũgũ hukubali mfuatano huu kama ilivyo katika lugha nyingine za Kibantu. Kwa mfano,
- andik –ĩr –w -a
andik –TDA –TDW -I
andikiwa
men -er –w -a
men –TDA –TDW -I
chukiwa
ob –er –w -a
ob –TDA –TDW -I
fungiwa
Mfuatano huu katika Kigĩchũgũ unakubaliana na mfuatano wa Kiolezo kama anavyourejelea Asiimwe (2011) jinsi ulivyopendekezwa na Hyman (2003) yaani kauli ya kutendea hutangulia kauli ya kutendwa. Hii ina maana kuwa mofimu katika kauli ya kutendea hufanganishwa kwenye mzizi kwanza ikifuatwa na mofimu katika kauli ya kutendwa. Mfuatano huu katika Kigĩchũgũ ulitumiwa kuonyeha kuwa kitendo fulani kilifanywa kwa niaba ya mtu au kitu.
Kauli ya Kutendea na kauli ya Kutendua (TDA+TDU)
Kigĩchũgũ huambikwa mofimu {-ĩr-} na {-er-} katika kauli ya kutendea na mofimu {-ũr-} na {-or-} katika kauli ya kutendua. Mofimu hizi huweza kufuatana katika Kigĩchũgũ ingawa mfuatano hukiuka uliopendekezwa na Hyman (2003). Hii ni kwa sababu Hyman (mtaje) alipendekeza mfuatano wa utendea kuja kabla kutendua lakini mfuatano huu katika Kigĩchũgũ huanza kwa kauli ya kutendua ikifuatwa na kauli ya kutendea. Kwa mfano,
ob –or –er -a
ob –TDU –TDA -I
fungulia
bat –ũr -ĩr -a
bat –TDU –TDA -I
kwamulia
tum –ũr –ĩr -a
tum –TDU –TDA -I
shonolea
Kutokana na mifano hii, ni dhahiri kwamba Kigĩchũgũ hukubali mfuatano wa kauli ya kutendea na kutendua. Kimantiki, kauli ya kutendua katika Kigĩchũgũ hutokea kabla ya kauli ya kutendea.
Kauli ya Kutendesha na Kutendea (TSH+TDA)
Mfuatano huu huchukua mofimu {-ithi-} na {-i-} katika kauli ya kutendesha katika Kigĩchũgũ na mofimu {-ĩr-} katika kauli ya kutendea. Kwa mfano,
end –ith –ĩr –I -a
end –TSH –TDA –tsh -I
pendezea
rĩm –ith –ĩr –i -a
rĩm – TSH – TDA – tsh-I
lim-ish-i-a
bũr –ith –ĩr –i -a
bũr –TSH –TDA –tsh -I
pigishia
Katika mifano iliyotolewa, mofimu nyambulishi katika TSH inatengwa na mofimu ya TDA. Hii ni kwa sababu TSH huishia kwa irabu na vilevile kauli ya TDA huanza kwa irabu.
Kigĩchũgũ pia huwa na usababishi mfupi ambao huwakilishwa na mofimu {-i-}. Katika mfuatano huu kauli ya kutendea hutokea kabla ya kauli ya kutendesha kinyume na uliopendekezwa na Hyman (2003). Kwa mfano,
kom –er –i -a
kom –TDA –TSH -I
lalishia
unan –ĩr –i -a
unan –TDA –TSH –I
katishia
Kauli ya Kutendea na Kutendana (TDA+ TDN)
Katika Kigĩchũgũ, mofimu za TDA ni {-ĩr-} na {-er-} na mofimu za TDN ni {-an-}. Kama anavyoeleza Mburu (2011) lugha ya Gikuyu hukubali mfuatano wa TDA na TDN ingawa mfuatano huu hukiuka ule uliopendekezwa na Hyman (mtaje). Katika Kigĩchũgũ, maumbo haya hujitokeza kama ifuatavyo;
tem –an –ĩr -a
tem –TDN –TDA -I
katiana
gũr –an –ĩr -a
gur –TDN –TDA -I
nunuliana
rũg –an –ĩr -a
rũg –TDN –TDA -I
pikiana
Kauli ya kutendana huja kabla ya kauli ya kutendea katika Kigĩchũgũ. Kulingana na mfumo wa Hyman (2003), ingetarajiwa kuwa kauli ya kutendea ingetokea kabla ya kauli ya kutendana. Hii haiwezekani kwa kuwa kisemantiki vitenzi hivi havingeleta maana iliyokusudiwa ya kuonyesha kuwa watu fulani wametendeana kitendo kile kimoja. Mfuatano huu katika Kigĩchũgũ unadhihirisha kuwa mofimu moja pekee {-ĩr-} ya utendea ndio hutumiwa.
Kauli ya Kutendesha na Kutendwa (TSH+ TDW)
Kauli ya TSH na TDW huwakilishwa kwa mofimu {-ith-} na {-w-} katika Kigĩchũgũ. Kama ilivyobainika katika sehemu ya 4.4.2, irabu /u/ ambayo ndio umbo la ndani katika kauli TDW huyeyushwa na kuwa /w/. Hata hivyo, ilibainika kwamba irabu /u/ hutumiwa kama kinyambulishaji cha TDW katika vitenzi ambavyo mizizi yake huishia kwa irabu /i/. Mfuatano wa TSH na TDW katika Kigĩchũgũ ulionyeshwa ifuatavyo;
thom –ith -w -a
thom –TSH –TDW -I
someshwa
kiny –ith –w -a
kiny –TSH –TDW -I
fikishwa
rũgam –ith –w -a
rũgam -TSH –TDW -I
simamishwa
Mfuatano huu wa TSH na TDW unaaafiki uliopendekezwa na Hyman (2003) kimofolojia na kisemantiki.
Kauli ya Kutendesha na Kutendua (TSH+ TDU)
Mofimu nyambulishi za kutendesha na kutendua katika Kigĩchũgũ ni { -ith-} na {-ũr-} au {-or-}. Kisemantiki na kimofolojia, kauli ya kutendua huja kabla ya kauli ya kutendesha katika vitenzi vya Kigĩchũgũ. Kwa mfano,
bing –ũr –ithi -a
bing -TDU -TSH -I
fungulisha ( mlango)
ob –or –ithi -a
ob –TDU -TSH -I
fungulisha (kamba)
rog -or –ithi – a
rog –TDU -TSH -I
rogoesha
Katika mifano hii, mfuatano uliopendekezwa na Hyman (keshatajwa) wa kauli TSH kuja kabla ya kauli TDU umekiukwa ili kudumisha maana.
Kauli ya Kutendesha na Kutendana (TSH+ TDN)
Mfuatano wa kauli tendeshi na tendana hukubalika katika Kigĩchũgũ. Mofimu {-ithi-} na { -i-} hutumiwa katika TSH na mofimu {-an-} katika TDN. Kwa mfano,
ak –ith –an –i -a
ak –TSH –TDN –tsh -I
jengeshana
nyu –ith –an –I -a
nyu –TSH –TDN –tsh -I
nyweshana
nyit –ith –an –I -a
nyit –TSH –TDN –tsh -I
shikishana
Kutokana na mifano hii, ni dhahiri kwamba Kigĩchũgũ hukubali mfuatano wa TSH na TDN. Mfuatano wa mofimu hizi katika Kigĩchũgũ unakubali Kiolezo kuwa kauli tendeshi hutangulia kauli tendana kama unavyopendekezwa na Good (2005).
Kauli ya Kutendua na Kutendwa (TDU+ TDW)
Kauli ya TDU na TDW huwakilishwa na mofimu nyambulishi {-ũr-} au {- or-} katika kauli ya kutendua na {-w-} katika kauli ya kutendwa katika Kigĩchũgũ. Mifano hii inadhihirisha mfuatano huo.
kũnj –ũr –w -a
kũnj –TDU -TDW -I
kunjuliwa
bing –ũr –w -a
bing –TDU –TDW -I
funguliwa
ob –or –w -a
ob –TDU –TDW -I
funguliwa
Kutokana na mifano hii, kauli ya kutendwa huja baada ya kutendua katika unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ. Hata hivyo, mfuatano huu wa TDU na TDW haukubaliki katika baadhi ya vitenzi.
Kauli ya Kutendua na Kutendana (TDU+TDN)
Kigĩchũgũ, huruhusu mfuatano wa kauli ya TDU ambayo mofimu zake ni {-or-} na {-ũr-} na kauli ya TDN ambayo huwakilishwa na mofimu {-an-}. Katika mfuatano huu, kauli ya TDU huja kabla ya TDN. Mofimu hizi yaani {-or-} na {-an-} hujitokeza zikifuata vitenzi sielekezi katika Kigĩchũgũ kama inavyodhihirika katika mifano ifuatayo;
ob –or –an -a
ob –TDU –TDN -I
funguana
Rog –or –an -a
Rog –TDU –TDN -I
rogoana
Thik –ũr –an -a
Thik –TDU –TDN -I
Zikuana
Kauli ya kutendua na kutendeka
Mofimu nyambulishi katika kauli ya TDK na TDU ni {-ĩk-} au {-ek-} na {-or-} au{-ũr-}. Katika mfuatano wa vinyambulishi hivi katika Kigĩchũgũ, kauli ya TDU huja kabla ya TDK kama inavyoonyeshwa kwenye mifano ifuatayo;
ob-or-ek-a
ob-TDU-TDK-I
funguka
rog-or-ek-a
rog-TDU-TDK-I
rogoka
Kauli ya kutendesha na kutendeka
Kauli ya TSH huwakilishwa kwa viambishi {-ithi-} na kauli ya TDK huwakilishwa kwa viambishi {-ĩk-} au {-ek-}. Katika mfuatano wa vinyambulishi katika lugha ya Kigĩchũgũ, kauli ya TSH hupachikwa kwanza ikifuatwa na kauli ya TDK. Kwa mfano,
rĩm-ith-ĩk-i-a
rĩm-TSH-TDK-I
limishika
thom-ith-ĩk-i-a
thom-TSH-TDK-I
somesheka
Mfuatano wa Viambishi Nyambulishi Vitatu
Kigĩchũgũ vilevile hukubali mfuatano wa kauli tatu katika kitenzi kimoja kwa wakati mmoja. Mfuatano huu ulielezwa kama ifuatavyo;
Kauli ya Kutendesha , Kutendea na Kutendana (TSH+TDA+TDN)
Katika mfuatano wa kauli tatu, Kigĩchũgũ kinakubaliana na pendekezo la Hyman (2003) la TSH, TDA na TDN. Hata hivyo, mfuatano wa viambishi nyambulishi tatu katika Kigĩchũgũ unapingana na wa Hyman (kehatajwa) kwa kiasi kwa vile unaruhusu mpishano. Tokeo la mfuatano huu katika Kigĩchũgũ unakuwa TSH, TDN na TDA hivyo basi kuathiri maana ya kitenzi kama ilivyo katika mifano ifuatayo.
tham –ith –an –ĩr –i -a
tham –TSH –TDN –TDA –tsh -I
hamishiana
taar –ith –an –ĩr –i -I
taar –TSH –TDN –TDA –Tsh -I
chagulishiana
men –ith –an –ĩr –i -a
men –TSH –TDN –TDA –tsh -I
chukishiana
Kanuni ya utokeaji ya mfuatano huu ni kwamba TSH inajitokeza baada ya mzizi wa kitenzi ikifuatwa na TDN na baadaye TDA.
Kauli ya Kutendesha, Kutendana na Kutendwa (TSH+ TDN+ TDW)
Kauli ya TSH, TDN na TDW zinaweza kufuatana kama Waweru (2011) anavyopendekeza. Katika mifano ifuatayo ya Kigĩchũgũ, pendekezo la mfuatano wa Hyman (2003) limeafikiwa. Hii ina maana kwamba kimofolojia kauli ya TSH huja baada ya mzizi, ikifuatwa na TDN kisha TDW ambayo huja mwishoni mwa kitenzi. Kwa mfano,
men –ith –an –w -a
men –TSH –TDN –TDW -I
kosanishwa
bũr –ith –an –w -a
bũr –TSH –TDN –TDW -I
piganishwa
andĩk –ith –an –w -a
andĩk –TSH –TDN –TDW -I
andikanishwa
Kauli ya Kutendesha, Kutendua na Kutendana (TSH+ TDU+ TDN)
Kigĩchũgũ hutumia mofimu nyambulishi {-ithi-} kuwakilisha kauli tendeshi, mofimu {-ũr-} na {-or-} katika kauli ya kutendua na mofimu {-an-} katika kauli ya kutendana. Mfuatano huu ni ule uliopendekezwa na Hyman (keshatajwa) ingawa kimofolojia Kigĩchũgũ kinaruhusu mpishano huru. Matokeo ya mfuatano huu kimofolojia katika Kigĩchũgũ ni kwamba kauli ya TDU huja baada ya mzizi wa kitenzi, ikifuatwa na kauli TSH na baadaye kauli ya TDN kama inavyodhihirika katika mifano.
ob –or –ith –an –i -a
ob –TDU -TSH –TDN –esh -I
fungulishana
thik –ũr –ith –an –i -a
thik –TDU –TSH -TDN -esh-I
zikulishana
kunj -ũr –ith –an –i -a
kunj –TDU –TSH –TDN –esh –I
kunjulishana
Kauli ya Kutendesha, Kutendea na Kutendwa (TSH+ TDA+TDW)
Kimofolojia, mfuatano wa kauli hizi ni TSH, TDA na TDW kama tu ilivyobainika katika Kigĩchũgũ. Kauli hizi huwakilishwa na mofimu tofauti kama ilivyoelezewa katika sehemu ya 4.4. mofimu hizi ni {-ithi-},{- ĩr-} au {-er-} na {-w-} ambayo muundo wake wa ndani ni {-u-} lakini hupitia uyeyushaji ili kuzuia mfuatano wa irabu mbili.Mfuatano huu katika Kigĩchũgũ ulionyeshwa kwa mifano ifuatayo;
ak –ith –ĩr –w -a
ak –TSH –TDA –TDW -I
jengeshewa
coker –ith –ĩr –w -a
coker –TSH –TDA –TDW -I
rudishiliwa
kũnj –ith –ĩr –w -a
kunj –TSH –TDA –TDW -I
kunjishiwa
Kauli ya kutendesha, kutendua na kutendwa (TSH+ TDU+ TDW)
Mfuatano huu unakubalika katika Kigĩchũgũ ingawa sio katika vitenzi vyote. Mfuatano huu huwa na mofimu ya TSH {-ith-}, TDU {-or-}m au {-ũr-} na TDW {-w-}. Mfuatano wa kimofolojia kama unavyodhihirishwa na mifano ya vitenzi katika Kigĩchũgũ ni kwamba kauli ya TDU hupachikwa kwanza baada ya mzizi, ikifuatwa na kauli ya TSH na baadaye kauli ya TDW. Kwa mfano,
bing –ũr –ith -w -a
bing –TDU –TSH –TDW -I
fungulishwa
kũnj –ũr –ith –w -a
kũnj –TDU -TSH –TDW -I
kunjulishwa
thik –ũr –ith –w -a
thik –TDU –TSH –TDW –I
*zikulishwa
Kauli ya Kutendesha , Kutendua na Kutendea (TSH+ TDU+ TDA)
Kigĩchũgũ hukubali mfuatano wa kauli ya TSH, TDU na TDA. Utaratibu wa mfuatano huu katika Kigĩchũgũ ni kwamba kauli ya TDU hujitokeza kwanza ambapo hupachikwa baada ya mzizi, ikifuatwa na kauli TSH na baadaye TDA. Mifano ifuatayo inadhihirisha mfuatano huo katika Kigĩchũgũ.
bing –ũr –ith –ĩr –i -a
bing –TDU –TSH –TDA -I
fungulishia
kũnj –ũr –ith –ĩr –i -a
kũnj –TDU –TSH –TDA -I
kunjulishia
ob –or –ith –ĩr –i -a
ob –TDU –TSH –TDA -I
fungulishia
thik –ũr –ith –ĩr –i -a
thik –TDU –TSH – TDA -I
zikulia
Kauli ya Kutendua, Kutendea na Kutendwa (TDU+ TDA+TDW)
Katika unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ, mfuatano huu hukubalika ambapo TDU hufuata moja kwa moja mzizi wa vitenzi. TDA hufuata TDU kwani huonyesha yambwa tendewa na baadaye TDW kama ilivyoonyeshwa katika mifano hii:
bing –ũr –ĩr –w -a
bing –TDU –TDA –TDW -I
funguliwa (mlango)
ob –or –er –w -a
ob –TDU –TDA –TDW -I
funguliwa (kamba)
tum –ũr –ĩr –w -a
tum –TDU –TDA –TDW -I
shonolewa
kũnj –ũr –ĩr –w -a
kunj –TDU –TDA –TDW -I
kunjuliwa
Kauli ya Kutendea, Kutendana na Kutendwa (TDA+ TDN+TDW)
Kigĩchũgũ hukubali mfuatano wa kauli TDA ambayo huwakilishwa kwa mofimu nyambulishi {-ĩr-} na {-er-}, kauli TDN ambayo mofimu yake ni{-an-} na kauli TDW ambayo huwakilishwa kwa mofimu {-w-}. Ingawa mfuatano huu ni kama ulivyopendekezwa na Hyman (2003), Kigĩchũgũ imeruhusu mpishano huru ambapo kauli ya TDN hufuata mzizi moja kwa moja , ikifuatwa na TDA na kisha TDW. Mfuatano huo umeonekana katika vitenzi kama ifuatavyo:
bũr –an –ĩr –w -a
bur –TDN –TDA –TDW -I
piganiwa
andĩk-an-ĩr-w-a
andĩk –TDN –TDA –TDW -I
andikaniwa
rum –an –ĩr –w –a
rum –TDN –TDA –TDW –I
tusianiwa
Kauli ya kutendua, kutendea na kutendana (TDU+ TDA+ TDN)
Mfuatano huu huwa na mofimu ya TDU {-ũr-} au {-or-}, TDA {-ĩr-} au {-er-} na TDN {-an-}. Mofimu hizi huambishwa kwenye mzizi wa vitenzi vya Kigĩchũgũ kwa mfuatano wa TDU –TDN -TDA. Mfuatano huu unakubalika katika Kigĩchũgũ ingawa sio katika vitenzi vyote kwani kauli ya TDU ambayo huonyesha kinyume cha kauli ya kutenda haijitokezi katika vitenzi vingi. Mifano ifuatayo inaonyesha mfuatano huo.
an –ũr –an –ĩr -a
an –TDU –TDN –TDA -I
anuliana
rog –or –an –ĩr -a
rog –TDU –TDN –TDA -I
rogoleana
tum –ũr –an –ĩr -a
tum –TDU –TDN –TDA -I
shonoleana
bing –ũr –an –ĩr -a
bing –TDU –TDN –TDA -I
funguliana
Mfuatano wa Viambishi Nyambulishi Vinne
Kigĩchũgũ ni mojawapo ya lugha za Kibantu zinazokubali mfuatano wa kauli nne. Kauli hizi ni kama vile;
Kauli ya Kutendesha, Kutendana, Kutendea na Kutendwa (TSH+ TDN+ TDA+ TDW)
Mfuatano wa vinyambulishi hivi katika Kigĩchũgũ ni TSH –TDN -TDA-TDW. Mfuatano huu ni kinyume na uliopendekezwa na Hyman (2003) na Good (2005) wa TSH –TDA -TDN na TDW. Mpishano huru katika Kigĩchũgũ umetokea ili kuleta kuhifadhi maana ya vitenzi. Mifano ifuatayo inadhihirisha hilo:
men –ith –an –ĩr –w -a
men –TSH –TDN –TDA –TDW -I
koseshanwa
bũr –ith -an –ĩr –w -a
bũr –TSH –TDN –TDA –TDW -I
pigishianwa
andĩk -ith -an –ĩr –w –a
andĩk –TSH –TDN –TDA –TDW –I
andikishianwa
Katika mifano hii, mofimu {-u-} ambayo huwa ni mofimu ya ndani katika kauli ya TDW imepitia uyeyushaji na kuwa {-w-} kwa vile imefuatana na irabu. Mifano hii husababisha kitenzi kuonekana kama vitenzi viwili vinavyokwenda sambamba hasa ikitumiwa katika sentensi. Kwa mfano,
- (a) Mwana wa Kamau nĩandikithanĩrwa nĩ Njoroge na Muthoni makĩandĩkana.
(b) Mtoto wa Kamau ameandikishianwa na Njoroge na Muthoni wakati wanapoandikana.
Katika sentensi hii, inaonekana kuwa Njoroge na Muthoni wanaandikana lakini wakati huohuo wanafanya kazi ya kumwandika mtoto wa Kamau.
Kauli ya Kutendua, Kutendesha, Kutendea na Kutendwa (TDU+ TSH+ TDA + TDW)
Kigĩchũgũ vilevile hukubali mfuatano wa kauli ya TDU –TSH -TDA na TDW kama inavyoonyeshwa katika mifano hii:
ob –or –ith –ĩr –w -a
ob –TDU -TSH –TDA –TDW -I
funguanishiwa ( kamba)
kũnj –ũr –ith –ĩr –w -a
kũnj –TDU –TSH –TDA –TDW -I
funguanishiwa
ak –ũr –ith –ĩr –w -a
ak –TDU –TSH –TDA –TDW -I
jengulishiwa
Mifano hii inadhihirisha wazi kuwa kauli mbalimbali zinaweza kufungamanishwa katika kitenzi kimoja na kuleta athari kisemantiki.
Kanuni za Mfuatano wa Viambishi Nyambulishi
Mfuatano wa viambishi nyambulishi kama wanavyosema Kihore, Massamba na Msanjila (2012) huongozwa na kanuni mbalimbali. Kanuni hizi ni kama vile:
Kanuni ya Kiambishi Nyambulishi {-w-}
Kama wanavyosema Kihore, Massamba na Msanjila (2012: 129), katika miandamano yoyote ya viambishi nyambulishi na mzizi wa vitenzi, kiambishi nyambulishi {-w-} lazima kitokee kama kiambishi nyambulishi cha mwisho pale inapobidi kitokee katika umbo la kitenzi. Hali hii ni sawa katika Kigĩchũgũ ambapo ilibainika kuwa kauli ya TDW ilitokea mwishoni mwa vitenzi katika mifuatano iliyojadiliwa. Kwa mfano,
andĩk-ĩr-w-a
caka-ith-an-w-a
cagũr-ith-an-ĩr-w-a
Mifano hii inaonyesha mfuatano wa kauli mbili, tatu na nne na katika mifuatano yote, kiambishi nyambulishi {-w-} kimetokea mwishoni mwa vitenzi.
Kanuni ya Viambishi Nyambulishi {-ĩr-} na {-er-}
Kanuni inaeleza kuwa mofimu {-ĩr}- na {-er-} hutumika baada ya mizizi ya vitenzi vinavyoishia kwa konsonanti katika vitenzi vya Kigĩchũgũ. Kwa mfano,
thom-er-a
thukum-ĩr-a
twar-ĩr-a
Vinyambulishi hivi vya kauli ya TDA hufauatana na kauli mbalimbali kama ilivyofafanuliwa
Kanuni ya Viambishi Nyambulishi Radidi
Kama wanavyosema Kihore, Massamba na Msanjila (2012: 130), kanuni ya viambishi nyambulishi radidi inasema kwamba upo uwezekano wa baadhi ya viambishi nyambulishi kurudiwa katika mwandamano katika umbo moja. Hali hii pia inajitokeza katika Kigĩchũgũ hasa mwandamano unaohusisha kauli ya TSH. Kwa mfano katika sehemu ya 4.5.1 (c)) TSH inapoandamana na TDA na TDN, urudiaji wa TSH hutokea. Kwa mfano,
andĩk –ith -ĩr -i -a
andĩk –TSH –TDA –TSH -I
andikishia
- nyw –ith –an –i -a
nyw –TSH –TDN –TSH -I
nyeshana
Vilevile katika sehemu ya mfuatano wa viambishi nyambulishi vitatu, (a) na (c), hali ya urudiaji wa TSH inajitokeza katika mfuatano wa TSH -TDN -TDA na TDU –TSH -TDN. Kwa mfano,
- tham –ith –an –ĩr –i -a
tham -ESH –AN -EA -ESH -I
hamishiana
- kũnj –ũr –ith –an –i -a
kunj -UA –ESH –AN –ESH -I
kunjulishana
Katika urudiaji huu mofimu {-i-}, ambayo huonyesha usababishi mfupi katika Kigĩchũgũ ndiyo iliyorudiwa. Kama anavyoeleza Wesana-Chomi (2013:73), kinyambulishi cha kauli ya TSH kinafaa kutokea kabla ya kinyambulishi cha kauli ya TDA na pia kabla ya kauli ya TDN.
Kanuni ya Kiambishi Nyambulishi {-an- }
Kama anavyosema Wesana-Chomi (2013:72), kiambishi kinyambulishi {-an-} hupachikwa kwenye vitenzi vyenye sifa maalumu tu ambavyo mizizi yake inaweza kupokea kinyambulishi {-an-}. Sifa hiyo ni kwamba kitenzi sharti kitaje tendo linalohusisha wahusika wawili au zaidi. Kila mhusika ni mtenda tendo na pia ni mtendwa. Katika vitenzi vya Kigĩchũgũ, kinyambulishi hiki kinaweza kutanguliwa na TDA, TSH na TDU katika mfuatano wa viambishi nyambulishi viwili kama ilivyoonyeshwa katika mfano (d), (g) na (i) au kikafuatana na viambishi nyambulishi vitatu na vinne kama ilivyo katika mifano wa mfuatano wa viambishi nyambulishi vitatu a,b na c.
Hitimisho
Makala hii imechanganua mofolojia ya unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ. Lengo kuu lilikuwa ni kufafanua mifanyiko iliyotumika katika unyambulishaji wa vitenzi hivyo, kujadili mfuatano wa viambishi nyambulishi na kutathmini kanuni zinazoruhusu au kuzuia mifuatano hiyo. Viambishi tamati katika unyambulishaji wa vitenzi vya Kigĩchũgũ vilijadiliwa katika kauli sita; kutendea, kutendwa, kutendesha, kutendana, kutendeka na kutendua. Katika uchanganuzi wa data, imedhihirika kwamba viambishi {-er-} na {-ĩr-} vilitumika katika kauli ya kutendea. Katika kauli ya kutendwa kiambishi {-w-} kilitumika kwenye mizizi ya vitenzi vilivyoishia kwa konsonanti na pia kiambishi {-u-} kilitumika katika baadhi ya vitenzi vya Kigĩchũgũ vilivyoishia kwa irabu. Kwa upande mwingine kauli ya kutendesha ilithihirishwa kwa viambishi viwili ambavyo ni {-ithi-} na {-i-}. Kiambishi {-an-} kilitumiwa katika kauli ya unyambulishaji ya kutendana. Kauli ya kutendeka ilitumia viambishi viwili vya unyambulishaji ambavyo ni {-ek-} na {-ĩk-}. Mwishowe kauli ya kutendua ambayo huonyesha kinyume cha vitenzi vya Kigĩchũgũ katika kauli ya kutenda ilijadiliwa. Ilithihirika kuwa kiambishi {-ũr-} ilitumika kuonyesha kauli hii.
Ilibainika kuwa kuna uchopekaji wa fonimu kama vile /r/ katika kauli ya unyambulishaji ya kutendea na /k/ katika kauli ya kutendeka. Uchopekaji huu ulitumikizwa ili kuhifadhi muundo wa K-V katika Kigĩchũgũ. Vilevile, uyeyushaji na udondoshaji wa irabu umetumikizwa ambapo katika kauli ya kutendwa irabu /u/ inayeyushwa na kuwa /w/ katika baadhi ya vitenzi vya Kigĩchũgũ vilivyoishia kwa irabu /i/ na kufuatwa na irabu /u/. Kwa upande mwingine katika kauli ya kutendwa, irabu /i/ ilidondolewa na irabu /u/ kuachwa kama kiambishi cha kauli hiyo ili kuzuia mfuatano wa irabu tatu na pia kuhifadhi maana ya vitenzi husika.
Vitenzi vya Kigĩchũgũ huweza kuambikwa viambishi vinyambulishi viwili, vitatu na vinne kwa wakati mmoja. Hali hii ni tofauti na lugha nyingine za Kibantu ambazo hukubali mfuatano hadi viambishi vitatu. Mifuatano iliyokubalika katika Kigĩchũgũ ilielezwa kulingana na kanuni ya Kioo kwa mujibu wa Baker (1985). Hata hivyo mpishano huru umeruhusiwa ambao ni kinyume na mfuatano wa Hyman (2003) ili kuhifadhi maana ya kitenzi.
MAREJELEO
Asiimwe, C. (2011). Unyambulishaji wa Vitenzi katika Lugha ya Runyankole. Tasnifu ya Uzamili. (haijachapishwa) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baker, M. (1985). The Mirror Principle and the Morpho-Syntactic Explanations. Linguistic Inquiry 16.3:373-415
Charwi, Z.M. (2013). Unyambulishaji na Dhana ya Uelekezi katika Lugha ya Kikuria, katika Omari, S na Peterson, R (wah). Kioo Cha Lugha. Vol 11, 2013. Taasisi ya Taaluma za Kiswahili: Dar es Salaam.
Chomsky, N. (1957). Syntactic Structure. The Hague: Muonton
Chomsky, N. (1988). Knowledge of Language, Its nature, Origin and age. New York: Praeger.
Gawasike, A. (2012). Dhana ya Uambikaji katika Kiswahili. Tasnifu ya Uzamili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. ( haijachapishwa)
Good, J. (2005). Reconstructing Morpheme Order in Bantu. The Case of Causativization and Applicativization. Diachronica 22: 3-57
Guthrie, M. (1967). Classification of the Bantu Languages. London: Pall Mall
Heine, B. na Mohlig, W.J.G.(ed) (1980). Language and Dialect Atlas of Kenya. Berlin: Dietrich Reimer Verlag.
Jepkoech, N.S. (2018). The Morphosyntax of the Keiyo Verb. (Unpublished M.A Thesis). Moi University
Katamba, F. and Stonham, J. (1993). Morphology. London: The Macmillan Press Ltd.
Kiango, J.G. (2008). Sarufi ya Vinyambuo Vitenzi vya Kiswahili: Mitazamo Mbalimbali kuhusu Kanuni za Unyambuaji, katika Ogechi, O.N. Shitemi, L.N. na Simala, K.I. (wah). Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Eldoret: Moi University Press.
Kihore, Y.M, Massamba, D.P.B na Msanjila Y.P. (2012). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA) Sekondari na Vyuo.Dar es salaam: TUKI.
Kiparsky, P. (1982). From Cyclic Phonology to Lexical Phonology. In Ver der Hulst and Smith (ed) The Structure of Phonological Representation. Dordrecht: Foris Publications.
Massamba, D.P.B, Kihore, Y.M. na Msanjila, Y.P. (2003). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu (fokisa).Dar es Salaam: TUKI.
Mutahi, K.E. (1983). Sound Change and Classification of Mt. Kenya Dialects. Berlin: Dietrich Reimes.
Ngowa, N.J. (2008). Mnyambuliko wa Vitenzi vya Kigryama. Tasnifu ya Uzamili. Chuo Kikuu cha Kenyatta. (haijachapishwa)
Schadeberg, T.C. (2003). Derivation, in Nurse,D and Philippson G.(eds.),.The Bantu Languages. London: Routledge.
Waithaka, N.M. (2009). Utohozi Mofolojia wa Maneno Mkopo ya Gikuyu kutoka Kiswahili. Tasnifu ya Uzamili.Chuo Kikuu cha Kenyatta (haijachapishwa)
Waweru, N.M. (2011). Gikuyu Verbal Extensions: A minimalist Analysis. (Unpublished PhD Thesis). Kenyatta University.
Wesana-Chomi, E. (2013). Kitangulizi cha Mofolojia ya Kiswahili.: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: TUKI
