Kiswahili na Familia za Mitaani: Nafasi yake katika Maendeleo ya Taifa la Kenya
Binyanya, Ruth, M. A Sirengo na S. Obuchi,
Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi
IKISIRI
Lugha na utamaduni ni vitu visivyotenganishika. Dhana ya utamaduni hurejelea hali ya maisha ya kila siku ya kikundi fulani katika jamii. Katika jamii za nchi ya Kenya, kunayo jamii ijulikanayo kama ya familia za mitaani au barabarani. Kutokana na majina yanayotumiwa kurejelea jamii hii, inaweza kuamuliwa moja kwa moja kuwa jamii hii ambayo vile vile inaunda jamii lugha haina chochote cha mno iwezayo kuchangia kwa jamii kubwa ya Kenya kwenye mahusiko ya maendeleo. Makala hii inachunguza jinsi familia za mitaani Kenya zinavyotumia Kiswahili katika ujenzi wa taifa hili. Lengo la makala hii ni kudhihirisha mikakati ya kimawasiliano iliyojengeka katika lugha ya Kiswahili katika kuwasiliana na umma mkubwa wa Wakenya kwa ajili ya maendeleo yake. Mbinu kuu ya ukusanyaji data itakuwa ni ya uchunguzi shiriki japo kutakuwa na mahojiano yatakayotumia sampuli ya kimaksudi. Nadharia ya Giles ya Maafikiano ya Mazungumzo itatumika katika uchanganuzi wa data.Utafiti huu utajikita katika jiji la Nairobi na tasnifu yake ni kuwa familia za mitaani zachangia maendeleo ya taifa la Kenya kupitia kwa lugha ya Kiswahili inayotumiwa nazo kiufundi.
Utangulizi
Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi nchini Kenya (Katiba, 2010). Lugha ya Kiswahili hutumiwa katika mawasiliano mapana hasa katika miji ya nchi ya Kenya. Mjini Nairobi, Kiswahili ni lugha sambazi (Githiora, 2002). Pia, Kiswahili ni somo la lazima katika shule za msingi na za upili za nchi ya Kenya. Haya yanadhihirisha kuwa lugha ya Kiswahili ni muhimu katika ujenzi wa taifa la Kenya. Matumizi ya lugha ya Kiswahili huchangia katika kukuza na kuendeleza umoja na utangamano wa taifa la Kenya. Familia za mitaani hujipata katika hali mbalimbali. Wakati fulani fulani wao huwasiliana na umma mpana. Mahusiano miongoni mwa familia za mitaani na pia baina yao na watu wengine hudhihirisha uteuzi wa lugha watakayoitumia. Familia za mitaani ni kikundi cha kijamii cha kipekee kwa namna wanavyoteua lugha ya kuwasiliana kwayo kutegemea wanazungumza na nani, wako wapi na azma yao ni ipi. Lugha ambayo itatumika katika muktadha fulani hukusudiwa kuwezesha watu kutekeleza nia zao za wakati husika. Familia za mitaani huwasiliana wao kwa wao, huwasiliana na wafanyibiashara na wapita njia. Mazungumzo baina ya familia za mitaani hudhihirisha upekee wa kikundi cha kijamii. Familia za mitaani huwa na lugha yao ya kuwasiliana ambayo hutenga makundi mengine ya kijamii. Mawasiliano baina yao na umma mpana wa Wakenya hudhihirisha matumizi ya lugha ya Kiswahili. Watu wa taifa la Kenya huwasiliana kwa mitindo mbalimbali wanapotumia lugha ya Kiswahili kutegemea tajriba zao. Kwa mujibu wa wayasemayo Short na Leech (1981), matumizi ya lugha ya mtu hutegemea tajriba yake ya maisha. Familia za mitaani za jiji la Nairobi zina namna zake za kuzungumza. Uteuzi wao wa elementi za kimuundo kama vile misamiati hutegemea muktadha wa matumizi pamoja na masiala mengine ya kijamii na kitamaduni.
Lugha ni suala la kijamii na haiwezi kutenganishwa na jamii husika (Leech, 1969). Makundi tofauti tofauti hutumia lugha kwa njia inayoyatambulisha kama makundi ya kipekee. Familia za mitaani huweza kutambuliwa kutokana na tabia zingine kukiwemo lugha yao. Familia za mitaani hulazimika kuteua lugha watakayoitumia kwa mujibu wa muktadha wa mazungumzo na nia zao za wakati husika. Lugha watakayoiteua ni ile itakayowawezesha kutimiza malengo yao kutegemea wanazungumza na nani, lini, wakati gani na wanataka nini. Lugha inayoelekea kutumiwa na makundi mbalimbali ya kijamii nchini Kenya ni Kiswahili. Habwe (1999), akiunga mkono hoja hii anasema kuwa Kiswahili sanifu ni lugha ya taifa la Kenya. Anaendelea kusema kwamba Kiswahili ndio lugha inayotumiwa katika mawasiliano ya kawaida na watu kutoka matabaka mbalimbali. Fishman (1968) naye anasema kuwa muktadha wa mahusiano baina au miongoni mwa washiriki mawasiliano huchochea matumizi ya aina fulani ya lugha. Anaonyesha kuwa muktadha huwafanya watu kutumia lugha ile ile kwa njia tofauti tofauti. Kwa misingi hii, makala haya yananuia kuonyesha namna familia za mitaani hutumia lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa muktadha wa matumizi katika suala zima la maendeleo ya taifa la Kenya. Lengo hili la makala haya linahusiana na namna familia za mitaani jijini Nairobi hutumia Kiswahili katika maendeleo na ujenzi wa taifa la Kenya katika ujumla wake.
Jiji la Nairobi na Hali ya Kilugha
Nairobi ndio mji mkuu nchini Kenya. Ni mji ulio na watu zaidi ya milioni 2.5. Idadi hii inaendelea kuongezeka kila uchao kutokana na uhamiaji wa mijini kutoka mashambani. Kwa sababu hii, huu ni mji ulio na watu kutoka jamiilugha mbalimbali. Nairobi ni mji ulio na idadi kubwa ya familia za mitaani ikilinganishwa na miji mingine hapa nchini Kenya. Pia, familia hizi za mitaani huwa za jinsia zote – jinsia ya kike na ya kiume. Hali ya kutoka kwa jamiilugha mbalimbali huwafanya watu kuzuka na mbinu za mbalimbali za kuwasiliana ili kukidhi mahitaji ya wakati husika. Familia za mitaani huwa na namna yao ya kuwasiliana ambayo hudhihirisha upekee wa kikundi. Familia za mitaani mjini Nairobi hutumia lugha yao ya mtaani ili kutenga makundi mengine ya kijamii na pia hutumia Kiswahili wanapowasiliana na umma mpana. Watafiti mbalimbali wamekuwa na machukulio ambayo yameonyesha kuwa familia za mitaani za jiji la Nairobi hutumia Sheng’ kuwasiliana (Abdulaziz na Osinde, 1997, Spyropoulos, 1987 na Githiora, 2002). Hata hivyo, familia za mitaani za jiji la Nairobi huwasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili hasa wanapowasiliana na umma mpana mbali na ukweli kuwa wanazo lugha zingine wanazozitumia katika mawasiliano yasiyokuwa mapana au ya kitaifa.
Katika mji wa Nairobi, familia za mitaani hupatikana katika maeneo mbalimbali ila wao hujumuika katika sehemu mahsusi. Sehemu hizi ni kama vile Bus Station, Afya Centre, Muthurwa, Railways, Country Bus, Gekomba, River Road, Kirinyaga Road na Ngara. Hizi ni sehemu za biashara mbalimbali, ikiwemo uuzaji wa matunda, mboga na nguo. Sehemu hizi hutembelewa na watu mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa ndipo magari hubebea abiria. Katika sehemu hizi, familia za mitaani huwasiliana na watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii. Ili kufaulisha shughuli hii ya kimawasiliano, lugha itakayoteuliwa kutumika ni muhimu kwa kutekeleza nia za wakati husika za familia za mitaani. Lugha hii inatokea kuwa ni Kiswahili. Nairobi ni mji ulio na ukwasi wa data kwa ajili ya makala haya.
Suala la Utafiti
Uwepo wa jamiilugha mbalimbali jijini Nairobi huchochea matumizi ya lugha itakayoeleweka na watu wa makundi mbalimbali ya kijamii. Muktadha wa mazungumzo huzua uteuzi wa lugha fulani fulani na wala si zingine. Uteuzi wa lugha itakayotumiwa na mtu fulani au/ na kikundi fulani cha kijamii huchochewa na masuala kama unazungumza na nani, wapi na kwa nia ipi. Utambulisho wa kijamii pia ni kichocheo cha matumizi ya lugha kwa njia fulani. Kama ilivyokwisha kutajwa, familia za mitaani huhusishwa na matumizi ya Sheng’ kwa nia ya kutenga watu wengine. Hata hivyo, kikundi hiki cha kijamii huwasiliana na watu wengine wasioelewa Sheng’ ya familia za mitaani. Mathalani, familia za mitaani huwasiliana na wafanyibiashara wakati wa kuwabebea mizigo, wenye magari na wapita njia. Kutokana na kuwasiliana na washiriki wa mazungumzo kutoka makundi tofautitofauti ya kijamii, lugha ya Kiswahili hutumika kwa kuwa ndiyo lingua franka ya taifa la Kenya kwenye ngazi ya kitaifa.
Familia za mitaani huishi maisha duni kama asemavyo Suda, (1997). Hali hii ya maisha duni huwafanya kutafuta mbinu mbalimbali za kujizoazoa na kuishi. Mbinu mojawapo ni uteuzi wa lugha itakayowawezesha aidha kupata msaada kutoka kwa wapiti njia au kazi ya kufanya. Lugha inayoelekea kutumiwa na watu mbalimbali jijini Nairobi na nchini Kenya kwa jumla ni Kiswahili. Namna familia za mitaani hutumia lugha ya Kiswahii hudhihirisha upekee wa kikundi hiki cha kijamii. Hili litatuwezesha kujibu maswali yafuatayo:
- Je, uamilifu wa lugha ya Kiswahili ni upi miongoni mwa familia za mitaani za jiji la Nairobi?
- Je, ni hali zipi za kimawasiliano ambazo huchochea matumizi ya lugha ya Kiswahili?
- Je, matumizi ya lugha ya Kiswahili yanaweza kutumiwa kudhihirisha upekee wa kikundi cha kijamii kwa kuwafanya kuwa ama kama kundi-ndani au kundi-nje kwa wenye kukitumia?
- Je, familia za mitaani huzingatia Kiswahili sanifu au la? Je, wao hutumia misamiati ya kubuni au iliopo katika Kiswahili sanifu na kwa nini?
Msingi wa Kinadharia
Makala haya yamejikita katika nadharia ambayo imetuwezesha kuchunguza namna familia za mitaani huwasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Nadharia hii imeweza kushughulikiwa katika vipindi mbalimbali kiwakati. Hata hivyo, makala haya yamefuata mkabala wa 1991. Nadharia ya maafikiano ya mazungumzo imetufaa katika kuchanganua data.
Nadharia ya maafikiano ya mazungumzo iliasisiwa na Giles mwaka wa 1973 na akaishughulikia tenamwaka wa 1975. Hata hivyo, nadharia ya maafikiano ya mazungumzo imeweza kukua na kuendelea kiwakati. Nadharia hii imeweza kushughulikiwa na wasomi mbalimbali na kuipa sura mbalimbali. Giles na Coupland, J. na Coupland, N. (1991) wanasema kuwa nadharia hii imeacha mtindo wa kuzingatia masuala mahsusi ya kiisimu wakati wa kuchunguza kikundi cha kijamii. Kulingana na wasomi hawa, msisitizo sasa ni kuchunguza masuala yote yanayohusiana na maafikiano baina ya wanakikundi ikiwemo viziada lugha kama vile ishara za mwili. Hii ina maana kwamba mtafiti anapaswa kuzingatia namna kikundi cha kijamii kinavyozungumza na ishara zingine za mwili ambazo hujitokeza wakati wa mazungumzo.
Katika mwaka wa 1973, Giles alishughulikia kile kisemwacho tu na wanakikundi. Anaona maafikiano kama mchakato wa ubadilishaji lugha baina ya wanakikundi. Mchakato huu hutumika kuwili: mwingiano na ulahajishaji. Katika hali ya mwingiano, mzungumzaji hutumia lugha ambayo huashiria maafikiano ya kikundi husika. Maafikiano husaidia katika kudumisha umoja wa kikundi. Katika mwingiano wa lugha, washiriki hufanana sana katika lugha wanayoitumia. Nadharia ya maafikiano ya mazungummzo inachukulia mwingiano kama ubadilishaji wa kijamii pale ambapo washiriki hugharamika ili kupata faida fulani ambayo yaweza kuwa ni kifaa muhimu cha kukubalika kijamii. Aina ya pili ya maaafikiano ni ulahajishaji. Hapa mzungumzaji hujitofautisha kilugha na washiriki wengine kwa kutumia lugha kwa njia tofauti ili asijitambulishe na kundi hilo.
Giles alijikita katika vipera vitatu ambavyo ni: mvuto wa mfanano, ubadilishaji wa kijamii na utambulisho wa kijamii. Anasema kuwa katika mvuto wa mfanano, mtu hujaribu kumbadilisha mwingine ili kuingiliana naye kwa kupunguza tofauti baina yao. Hapa wazungumzaji huafikiana kilugha. Mvuto huu wa mfanano husababisha ubadilishaji lugha kwa jamii ili mtu aweze kuzungumza kama wenzake na hivyo kutambuliwa kama mmoja wao. Maoni ya Giles yanaonyesha kuwa mtu huzungumza kamawenzake katika kikundi husika kama mbinu ya kukubalika katika kikundi hicho.
Coupland, N. na Coupland, J. walishirikiana na Giles, H. na kuiangazia nadharia ya maafikiano ya mazungumzo katika mwaka wa 1991. Wasomi hawa walijikita zaidi katika suala la muktadha wa mahusiano ya washiriki wa mazungumzo. Wanasema kuwa muktadha wa mazungumzo huchochea mabadiliko katika lugha itakayotumiwa, misimbo, mtindo wa kuzungumza na uteuzi wa mbinu mwafaka ya kuishi. Hii inaonyesha kuwa, mbinu za kuishi huchochea wazungumzaji kuteua lugha faafu kwa mujibu wa muktadha.
Wasomi hawa wanasema kuwa maafikiano huweza kujitokeza katika viwango viwili. Viwango hivi nimpangilio na uchangamano wa muktadha na maafikiano ya kikundi. Uchangamano wa muktadha huwafanya wazungumzaji wa ana kwa ana kutafuta njia mbadala ya kuwasiliana. Hii hudhihirisha umoja wa kikundi cha kijamii. Katika kiwango cha pili wanasema kuwa mbinu ya kuafikiana hudhihirisha mabadiliko ya misimbo, au uteuzi wa lugha. Wanasema kuwa uteuzi wa lugha itakayotumiwa katika mazungumzo unahusiana na imani za wanakikundi, mitazamo yao na hali zinazowakumba. Kwamba, wanakikundi wa wingi-lugha huamua lugha ipi itumike katika muktadha upi. Hii inaonyesha kuwa watu kikundi cha kijamii hutumia lugha mahsusi kwa nia mahsusi.
Wasomi hawa wanaelezea pia masuala ya mwingiano na ulahajishaji baina ya wanakikundi. Hata hivyo, wanaonyesha maoni tofauti kuhusu mwingiano na ulahajishaji. Katika mwingiano, Giles, (1973) alijikita katika mvuto wa mfanano, ubadilishaji wa kijamii na utambulisho wa kijamii ila katika mwaka wa 1991, Giles na wenzake wanauchukulia mwingiano kama njia ya utangamano wa kijamii au utambulisho. Katika mwaka wa 1973, Giles anaona mwingiano kama mchakato wa kubadilisha lugha na kisha watu wengine katika kundi hilo hufuata mtindo uo huo. Katika mwaka wa 1991, Giles na wenzake wanasema kuwa watu huafikiana kimazungumzo na kitabia kwa sababu ya: chukulizi kuhusu kikundi hicho cha kijamii, namna wanavyotaka kueleweka na umma mpana, faida watakayopata, mazoea ya jamii, nia zao na viwango vya mazungumzo. Maoni haya yanatofautiana na aliyoyazungumzia Giles mwaka wa 1973. Namna wanavyotaka kueleweka na faida watakayopata kutokana na kuafikiana huwafanya wanakikundi kuteua lugha itakayofaa katika mazungumzo hayo. Mazoea ya jamii na nia za wazungumzaji huwafanya kuteua lugha na misamiati inayoeleweka na washiriki wa mazungumzo hayo. Chukulizi kuhusu kikundi husika huwafanya wanakikundi kuteua lugha mbadala ili kupunguza chukulizi hasi. Maoni ya wasomi hawa yanadhihirisha kuwa uteuzi wa lugha itakayotumika katika mazungumzo fulani huchochewa na muktadha wa mazungumzo.
Giles na Coupland wanasema kuwa ulahajishaji huwa mbinu ya kukabiliana na hali ya wakati husika kinyume na Giles, (1973) ambaye alidai kuwa ulahajishaji hutokana na kutotaka kuhusishwa na kundi husika. Giles, H. na Coupland, J. na Coupland, N. (1991) wanaonyesha kuwa ulahajishaji huweza kutokea hapa na pale kwa mtu wa kikundi fulani kutegemea nia yake ya mazungumzo. Kwamba, yule anayejitenga na wanakikundi wengine hufanya hivyo ili kuchukuliwa kwa njia chanya na watu wa makundi mengine. Kwao, ulahajishaji hauwezi kuepukika katika hali fulanifulani. Kwamba, muktadha huweza kuwafanya watu wa kikundi fulani cha kijamii kujitenga na namna walivyozoeleka. Wanakikundi hubadilisha lugha kwa nia ya kubadilisha mitazamo ya watu wa makundi mengine kuwahusu.
Mazungumzo baina ya watu kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii huzua haja ya kuteua lugha itakayoeleweka na washiriki wa mazungumzo hayo. Familia za mitaani hujipata katika miktadha mbalimbali. Miktadha mingine huwafanya kutumia lugha inayowatambulisha wao ilikutenga makundi mengine ya kijamii. Giles, Coupland, N. na Coupland, J. (ibid) wanazungumzia aina za miktadha. Wanadai kuwa miktadha changamano huwafanya watu kutumia lugha itakayowawezesha kupata suluhu. Wakati mwingine, familia za mitaani hulazimika kuomba msaada. Watahitajika kutumia lugha itakayoeleweka na washiriki wa mazungumzo hayo. Familia za mitaani pia huzungumza wao kwa wao. Inaelekea kuwa, mazungumzo baina yao yatahusisha lugha yao ya ‘mtaa’ ilhali wanapozungumza na watu kutoka makundi mengine watatumia lugha ya Kiswahili. Nadharia hii ya maafikiano imetufaa katika kuchunguza namna ambavyo familia za mitaani huwasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa mujibu wa muktadha. Tumejikita katika maoni ya Giles, H, Coupland, J. na Coupland, N. ya mwaka wa 1991.
Mbinu Za Utafiti
Tasnifu hii itatumia mbinu mbili katika kukusanya data. Mbinu hizi ni uchunguzi shiriki na mahojiano. Tutakwenda nyanjani ambapo tutajenga uhusiano mzuri baina yetu na familia za mitaani ili washirikiane nasi. Katika mahojiano, tutatumia maswali yasiyoratibishwa ili kuruhusu mazungumzo yatakayotuwezesha kupata data tosha. Tutapanga wakati wa kukutana nao kwa kuzingatia wakati wao mwafaka. Saldana, (2011) anasema kuwa wakati wa utafiti, mtafiti azingatie wakati mwafaka wa watafitiwa na wala sio wakati mwafaka wa mtafiti. Familia za mitaani huhamahama kutoka sehemu moja hadi nyingine na kwa sababu hii, tutalazimika kuwatafuta wanapopatikana. Tutagawa sehemu ambazo hukisiwa kuwa familia za mitaani hupenda kukutana katika makundi sita ifuatavyo:
- Sehemu ya Bus Station na Afya Centre
- Muthurwa na Railways
- Country Bus na Gekomba
- River Road na Kirinyaga Road
- Ngara
- Globe Cinema na Jeevanjee
Matokeo na Mjadala
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa familia za mitaani jijini Nairobi hutumia lugha ya Kiswahili katika takribani shughuli zao zote. Hali hii inatokana na hali ya Kiswahili kuwa lugha ya taifa na vile vile hali ya wanafamilia za mitaani kuwa wanatokea jamiilugha zote za nchini Kenya. Hata hivyo, utafiti huu umeweza kubaini kuwa nyingi katika familia hizi za mitaani zatokana na jamii lugha ya Kikuyu. Kwa mujibu wa shirika la Consortium of Street Children (CSC), familia za mitaani za jiji la Nairobi zinahusisha asilimia 46 ya jamiilugha ya wakikuyu na asilimia 54 ni kutoka jamiilugha nyingine za nchi ya Kenya. Sababu mojawapo ya hali kuwa hivi ni ukaribu wa Wakikuyu kwa jiji la Nairobi. Japo hivi ndivyo hali halisi ilivyo, inapokuja kwa kuwasiliana lugha inayotawala mawasiliano ni Kiswahili. Haikosi hali hii ya kudumisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yatokana na kule kutaka kujibainisha kama kundi ndani lisilojua ukabila. Uvunjaji wa ukabila ni moja katika nguzo kuu zipelekeazo kupatikana kwa maendeleo ulimwenguni kote kama inavyodhihirishwa na mataifa yaliyo na hali ya umoja lugha kama vile Korea, Uchina na Marekani.
Familia za mitaani Kenya, na hasa jijini Nairobi, hazitumii Kiswahili cha aina moja kwa mawasiliano. Hali ya Kiswahili kipi kitumike wapi, lini, kwa nani na kwa athari gani huendana na masiala mbali mbali ya kijamii na kiuchumi. Kwa mfano, wanafamilia za mitaani wanapokuwa wanawasiliana wenyewe kwa wenyewe wanatumia aina ya Kiswahili wanachokitaja wenyewe kuwa ni Kiswahili Kinairobi. Kwa mfano;
Mtu 1: Sasa, umepotea!
Mtu 2: Ni wewe ndio umepotea, huonekani bwana!
Mtu 1: Sisi tuko, ni maubao tu saa ii na sijapata kakitu.
Mtu 2: Hauna hata ya mandanyo?
Mtu 1: Niko na mbao na nimekosa mbao ingine ndio nibuy chai na mandazi.
Mtu 2: Twende nikuokolee.
Katika mazungumzo haya, familia za mitaani wametumia lugha ya Kiswahili-kinairobi. Wametumia maneno kama vile maubao kwa maana ya njaa, mandanyo ni mandazi, mbao ni shilingi ishirini na nikuokolee kwa maana ya kusaidiwa. Mazungumzo baina ya familia za mitaani yanadhihirisha upekee wa kikundi hiki cha kijamii. Upekee huu unawafanya kuwa kundi-ndani kama tulivyoonyesha kwenye mazungumzo yao. Familia za mitaani huzungumza kwa namna tulivyoonyesha katika miktadha fulani fulani. Utafiti huu ulibaini kuwa familia za mitaani huwasiliana kwa kutumia Kiswahili-kinairobi wanapowasiliana na watu waliozoeana nao. Mazungumzo ya aina hii huwa ya kawaida wala si rasmi na hutofautiana na mazungumzo baina yao na maafisa wa kaunti au maafisa wa polisi. Hali hii pia huwa tofauti pale ambapo wanaomba usaidizi kutoka kwa watu wenye magari barabarani. Familia za mitaani wanapozungumza na wenye magari hujibidiisha kutumia Kiswahili kinachokubalika na wote katika jamii ya Kenya na kiwezacho kusahilisha mawasiliano kwa wote. Hali hii pia hutokea pale ambapo wanafamilia za mitaani wanaomba vibarua kutoka kwa wafanya biashara. Mazungumzo yafuatayo ni baina ya mmoja wa familia za mitaani na mfanyabiashara (MB) katika eneo la Muthurwa.
MB: Nyinyi, ninataka kuwatuma.
Mtu 3: Wapi mama?
MB: Kwa stoo yangu.
Mtu 4: Hapo sawa, lakini mara hii utulipe vizuri kidogo.
Mtu 3: Ile stoo yako unajua iko mbali halafu watu wanasongamana sana kwa hiyo njia.
MB: Endeni haraka kastoma wasipate sina vitu za kuwauzia.
Mtu 3: Ule jamaa atatutolea kweli au atakataa tena?
MB: Ninampigia simu saa ii ii.
Mazungumzo baina ya mfanya biashara na vijana hawa wa familia za mitaani yanaonyesha matumizi ya Kiswahili ambacho kinaelekea kuwa sanifu. Vijana hawa wa familia za mitaani hawajatumia lugha yao ya mitaani. Hii ni kwa sababu wanawasiliana na mtu kutoka kikundi kingine cha kijamii. Katika mawasiliano haya, familia za mitaani wametumia msimbo pana ili kueleweka na washiriki wote wa mazungumzo haya. Ilifahamika kuwa wafanya biashara huwasiliana na familia za mitaani kwa kutumia lugha ya Kiswahili ili kusahilisha mawasiliano. Mazungumzo baina ya familia za mitaani na mfanya biashara yanadhihirisha tofauti katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Mazungumzo haya yanaonyesha kuwa familia za mitaani wanazingatia sarufi na wanaendeleza maneno ipasavyo. Familia za mitaani wametumia maneno kama vile ‘hii’ ilhali mfanya biashara analitamka ‘ii’. Hii ni ithibati tosha kuwa familia za mitaani wanaweza kuwasiliana kwa kutumia Kiswahili kwa ufasaha. Mfano mwingine wa matumizi ya lugha kwa ufasaha ni mazungumzo yafuatayo baina ya familia za mitaani na afisa wa kaunti. Afisa wa kaunti alikuwa na jukumu la kuondoa familia za mitaani katika eneo la mkahawa mtaani Ngara. Familia za mitaani hawakuwa radhi kuondoka maana ilikuwa usiku. Mazungumzo yao ni kama ifuatavyo;
Afisa wa kaunti: (akichukuwa gunia la kutoka kwa mmoja wa familia za mitaani) tokeni hapa, mnaharibia watu biashara zao. Nenda mahali mmezoea.
Mtu 5: Siendi, siendi na siendi. Kwani wewe hauna huruma?
Afisa wa kaunti: Wee, wee, nitakuumiza vibaya. Mtaenda cell saa ii.
Mtu 6: Sasa sisi hatuna kazi, kazi ni kushinda tumeshikwashikwa tu kiujinga tu. Ujinga tu.
Mtu 7: (mwanamke) Wewe, kama hauna mahali pa kulala, sema nikusongee. Nita……..
Afisa wa kaunti: Tokeni hapa, tokeni, toka, mahali pa kulala nini?
Mtu 7: Enda huko, kwanza leta tandiko yangu, (akijaribu kumnyanganya afisa wa kaunti gunia). Au kuja nikusongee tulale. Kuja, kuja kama unataka nikusongee.
Afisa wa kaunti: Ninakuanga na kitanda na mattress kubwa na poa kuliko hii uchafu yako.
Mtu 7: Na unafanya nini hapa saa hii? Unataka nitoe nguo, nitoe zote? (Afisa wa kaunti anarusha gunia chini na kuondoka kwa haraka)
Mazungumzo haya yalihusisha familia za mitaani za jinsia ya kike na kiume na afisa wa kaunti ya Nairobi. Imedhihirika wazi kuwa familia za mitaani wanarudiarudia baadhi ya vitenzi kwa nia ya kusisitiza. Hii ni sifa mojawapo inayowatambulisha kama kikundi cha kijamii chenye upekee katika matumizi yao ya lugha. Kwa mfano Mtu 5 anarudia neno ‘siendi’ kuonyesha msisitizo kuwa hatatoka mahali hapo. Pia, familia za mitaani wametumia neno ‘wewe’ ipasavyo kinyume na afisa wa kaunti anayetumia neno ‘wee’. Kwa hali hii, ni wazi kuwa familia za mitaani wanakitumia Kiswahili kwa ufasaha hasa wanapozungumza na watu kutoka makundi mengine ya kijamii. Sababu kuu ya kutumia Kiswahili kwa ufasaha wanapowasiliana na baadhi ya watu ni kutaka kujitenga na namna watu walivyowazoea kuwa wao hawajui Kiswahili sanifu. Mbinu hii ya kutumia Kiswahili kwa ufasaha huwafanya kuwa kundi-nje kwa muda mfupi. Huu ni mkakati mojawapo wa kuishi mitaani. Kwamba, familia za mitaani huweza kutumia Kiswahili sanifu hasa kutegemea wanazungumza na nani. Wakati mwingine familia za mitaani hulazimika kujitenga na lugha yao ya mitaani ili kusahilisha mawasiliano au pia kwa nia ya kujibainisha na kundi lao kutokana na mtazamo hasi kuwahusu. Ingawa hivyo, kujibainisha huku ni kwa muda mfupi tu na hutegemea muktadha wa mazungumzo.
Halafu, ifahamike kuwa wapo wanafamilia za mitaani ambao japo wanaishi mitaani wamekwenda skuli na wanavyo vyeti. Watu kama hawa walionekana kama ambao Kiswahili chao kilielekea kuwa sanifu hasa kisintaksia na kifonolojia maana ndivyo viambajengo vya muundo wa lugha tulivyovishughulikia sana katika utafiti huu. Usanifu wa matumizi ya Kiswahili ulijibainisha zaidi wanafamilia hizi za mitaani walipowasiliana na polisi pamoja na maaskari wa jiji la Nairobi. Hali hii ilijitokeza kama mbinu ya kujinusuru na kujitofautisha na umma mkubwa wa wanafamilia za barabarani ambao huwa wasumbufu, waharibifu, wanyang’anyi na watenda maovu katika ujumla wake. Kimsingi, kama walivyodokeza watafitiwa wenyewe, hali hizi zote za matumizi ya lugha ya Kiswahili katika aina zake zote hupania kuleta maafikiano ya kimazungumzo na ni umoja huu wa kilugha uwezao kuchochea maendeleo ya taifa lolote lile likiwemo hili la Kenya. Mfano wa mmoja wa familia za mitaani aliyesoma ni Mtu 8 katika utafiti huu. Mazungumzo baina yake na afisa wa polisi ni kama ifuatavyo;
Afisa wa polisi: Kijana, utapelekwa kwenye rehab coz huko maisha ni poa kuliko hapa kwa street.
Mtu 8: Afande, hapa mitaani ni afadhali. Tunapata chakula na tuna uhuru wa kutosha.
Afisa wa polisi: Wewe ni ng’ombe ya wapi! Hujui shida iko mingi kwa street? Endelea kucheza, utapigwa risasi.
Mtu 8: Mimi si jambazi wala sijawahi kuiba. Nyinyi mna maonevu tu kwa chokoraa. Sio kupenda kwetu tunaishi hivi.
Mtu 9: Lakini Afande, si mnajua tu sisi si watu wabaya. Ni……..
Afisa wa polisi: Nyinyi ndio hamjisikii kusaidiwa. Hata mkipewa job, haya, tuseme niwapeleke kwangu mkanichungie ng’ombe si mtakaa siku moja mbili halafu mpotee. Kwani hii street inawafurahisha na nini? Kwenda huko.
Mazungumzo haya yanatofautiana na yale ya familia za mitaani na afisa wa kaunti. Afisa wa kaunti anazungumza nao kwa ukali. Familia za mitaani nao pia wanatumia ukali huo huo huku wakitumia Kiswahili kwa ufasaha. Mazungumzo baina ya afisa wa polisi na mtu 8 na mtu 9 yanadhihirisha matumizi ya Kiswahili sanifu kwa upande wa familia za mitaani. Mtu 8 ni mmoja wa familia za mitaani ambaye aliwaeleza watafiti kuwa alikuwa amesoma hadi kidato cha tatu. Kwamba alikuwa na mamake na waliishi na baba wa kambo. Wazazi walipokosana, mama akaondoka na kuwaacha watoto. Baba akamfukuza mtu 8 maana mamake alimzaa nje ya ndoa. Utengano huu ulimfanya mtu 8 kuacha masomo akiwa kidato cha tatu. Kijana huyu alizungumza Kiswahili kwa ufasaha. Inadhihirika kuwa hakuchanganya ndimi katika mazungumzo yake na afisa wa polisi. Anatumia neno ‘mtaani’ ilhali afisa wa polisi anatumia neno ‘street’. Afisa wa polisi anachanganya ndimi na hata kutaja baadhi ya maneno kwa ufupi kama vile ‘rehab’ kwa maana ya ‘Rehabilitation’ ilhali mtu 8 anatumia Kiswahili sanifu katika kurejelea sehemu na dhana mbalimbali. Mazungumzo haya yanaonyesha wazi kwamba familia za mitaani hutumia Kiswahili sanifu hasa wanapozungumza na maafisa wa polisi. Familia za mitaani huzungumza Kiswahili kwa ufasaha wanapozungumza na maafisa wa polisi kama mkakati wa kujitenga na kundi hili kwa muda mfupi. Inadaiwa kwamba maafisa wa polisi hawapendi kuzungumziwa kwa lugha ya mtaa ya familia za mitaani. Maafisa hawa huichukulia Sheng’ inayotumiwa na familia za mitaani kama lugha ya wakora. Ili kuepuka chukulizi hizi, familia za mitaani hutumia Kiswahili kwa ufasaha ili waweze kuelewana na maafisa wa polisi. Kwamba, matumizi ya lugha kwa ufasaha huwawezesha kutazamwa kwa njia chanya.
Mazungumzo baina ya familia za mitaani na maafisa wa polisi yanaonyesha kuwa uhusiano baina ya wazungumzaji ni kichocheo cha matumizi ya lugha kwa njia fulani. Familia za mitaani wanatumia Kiswahili kwa ufasaha wanapozungumza na maafisa wa polisi kinyume na wanapozungumza na maafisa wa kaunti. Mazungumzo baina ya familia za mitaani na maafisa wa kaunti (kama tulivyoonyesha) yanadhihirisha matumizi ya lugha isiyo na heshima. Mtu 7 anamwambia afisa wa kaunti kwa ukali kuwa iwapo hana mahali pa kulala atamsongea. Mazungumzo hayo pia yanadhihirisha kuwa familia za mitaani hutumia ukali wanapowasiliana na maafisa wa kaunti. Pia, ni wazi kuwa familia za mitaani hurudiarudia vitenzi katika mazungumzo yao. Hali hii inatokea kuwa kinyume katika mazungumzo baina ya maafisa wa polisi na familia za mitaani. Imedhihirika kuwa familia za mitaani za mitaani hutumia lugha ya upole wanapozungumza na maafisa wa polisi. Mtu 8 anatumia lugha fasaha na anazungumza kwa unyenyekevu katika mazungumzo baina yake na afisa wa polisi. Haya yote ni kutokana na uhusiano uliopo baina ya familia za mitaani na maafisa wa polisi kwa upande mmoja na familia za mitaani na maafisa wa kaunti kwa upande mwingine.
Utafiti huu umebainisha wazi kuwa zipo tofauti za matumizi ya lugha ya Kiswahili yanayoendana na masiala ya kijamii kukiwemo lile la umri na jinsia. Kwa jumla, wanafamilia za mitaani walio na umri wa miaka baina ya 18 na 40 hawatumii tasfida nyingi katika kutaja mambo ya aibu na usimbeko. Wao walionekana kuvitaja vitu jinsi vilivyo bila kuvivalisha nguo. Kwa upande mwingine, watoto na watu wa umri mkubwa walionyesha matumizi ya lugha ya Kiswahili yaliyo ya tahadhari kuu ili wasije wakaudhi wasikilizaji wao. Mhojiwa mmoja mzee alipoulizwa kuhusu hali hii ya matumizi ya lugha, alisema kuwa vijana wanatumia lugha kwa jinsi wanavyofanya kwa sababu ni limbukeni walio na nguvu nyingi na pupa za maisha. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa hali hii tunayoishuhudia kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa familia za mitaani ndiyo inayozipitikia familia zote ulimwenguni hapa (Davy, C 1978). Kwa hali hii, familia za mitaani jijini Nairobi ni kama familia nyingine yo yote ile inapokuja kwa suala la tasfida na matumizi ya lugha. Vile vile, utafiti huu umeonyesha kuwa kina dada walijitokeza kama ambao walitumia lugha yao kwa tahadhari kuu wakilinganishwa na wanaume. Mbali na kutumia lugha iliyojaa upole, kwingineko kina dada walionekana wakitumia lugha ishara badala ya lugha zungumzwa. Hapa tuna maana kuwa lau kama kina dada wangekuwa na maguvu kama walio nayo kina baba, wangesaidia sana katika ujenzi wa taifa ambao ungeleta maendeleo katika taifa hili la Kenya. Kule kunyamaza au kutumia ishara kwa kina dada katika kuwasiliana ni mkakati mwema wa kimawasiliano ambao humwepushia mhusika hali ya kuropokwa na kujisaliti kimawasiliano kwa kusema mambo yasiyohitajika.
Data kwa ajili ya utafiti huu ilipatikana kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi. Kutegemea wanakopatikana wanafamilia za mitaani, matumizi yao ya lugha ya Kiswahili yalijipambanua mbali na mikakati yao ya kimawasiliano pia kujitokeza wazi. Japo masafa yaliyopo baina ya Ngara na River Road pamoja na Kirinyaga Road sio ya mbali mno, ilijitokeza kuwa lugha ya Kiswahili iliyotumika Ngara ilikuwa ya upole ikilinganishwa na ile ya River Road na Kirinyaga Road. Kinachosisitizwa hapa ni kuwa maeneo ya kijiografia na kitabaka wanakoishi watu siku zote huwa na athari fulani kwa lugha na tabia za lugha husika. Hali hii hii ndiyo inayotupa matokeo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili ya familia za mitaani za Afya Centre na Bus Station yakitofautiana kwa ukali wa kimsamiati na wa toni. Kwa jumla, ilibainika kuwa hakuna familia za mitaani za eneo moja jijini Nairobi zilizokubalika kuhamia sehemu nyingine bila idhini na sababu maalumu. Kwa hiyo, familia hizi za mitaani huishi mahali fulani maalumu panapoonekana kuwa panafaa kwa ajili ya chakula kwa familia husika na pia kwa vibarua na ajira. Hali hii inawaepushia wanafamilia hizi hali ya kuwa ombaomba na badala yake kujitegemea kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa la Kenya kwa jumla.
Hitimisho
Fikira kwamba familia za mitaani ni kupe na za watu wanaolaza damu zimepitwa na wakati. Wanafamilia za mitaani ni watu walio na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa la Kenya kama walivyo Wakenya wengine. Moja katika njia ambazo kwazo maendeleo hayo ya taifa la Kenya yanaweza kuafikiwa ni kupitia kwa Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa la Kenya na vile vile hufundishwa na kutahiniwa katika mfumo wa elimu Kenya. Wanafamilia za mitaani jijini Nairobi huutumia ujuzi wao wa lugha ya Kiswahili ili kuendeleza shughuli zao za maisha ya kila siku na kama mkakati wa kuishi jijini. Kwa sababu hii, itakuwa vyema kama familia kama hizi zitaweza kuigwa na sekta zingine za umma wa Wakenya kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili la Kenya.
Marejeleo
Abdulaziz, M. na Osinde, K. (1997) Sheng’ and Engsh: Development of Mixed Codes among the Urban Youth in Kenya. In International Journal of the Sociology of Language 125 (Sociolinguistic Issuesi n Sub-Saharan Africa) pp.4 5-63.
Coupland, J. Coupland, N. na Giles, H. (1991) Contexts of Accommodation. New York: U.S.A. Cambridge University Press.
Fishman, J. (1968) Reading in the Sociology of Language. The Hague: Mouton and Co. N. V Publishers.
Giles, H. (1975) Speech Style and Social Evaluation. London: Academic Press Inc.
Githiora, C. (2002) Sheng: Peer Language, Swahili Dialect or Emerging Creole? Journal of African Cultural Studies, Vol. 15, No. 2, (Dec., 2002), pp. 159-181 Published by: Taylor & Francis, Ltd. Stable URL: http://www.jstor.org/stable/3181415
Habwe, J. (1999) Discourse Analysis of Swahili Political Speeches. Tasnifu ya Uzamifu ya Chuo Kikuu cha Nairobi ambayo haijachapishwa.
Leech, G.N na Short, M.H (1981) Style in Fiction. USA: Longman Group UK Limited.
Leech, G.N (1969) A Linguistic Guide to English Poetry. Edinburgh Gate: England: Pearson Education Limited
Saldana, J. (2011) Fundamentals of Qualitative Research. New York: Oxford University Press.
Suda, C. (1997) Street Children in Nairobi and the African Cultural Ideology of Kin-based Support System: Change and Challenge. Child Abuse Review Vol. 6.
Spyropoulos, M. (1987) Sheng: Some Preliminary Investigations into a Recently Emerged Nairobi Street Language. In Journal of the Anthropological Society of Oxford 18 (1): 125-136.
Download Kiswahili na Familia za Mitaani: Nafasi yake katika Maendeleo ya Taifa La Kenya